Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtandao wa Aga Khan unavyogusa wananchi Tanzania

Tue, 16 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mtukufu Aga Khan ameendelea kutafsiriwa katika maisha halisi ya wananchi kupitia shughuli za maendeleo zinazofanywa na Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) baada ya mamilioni ya Watanzania kunufaika na huduma zinazotolewa kupitia sekta mbalimbali nchini Tanzania

AKDN ni muungano wa mashirika binafsi ya kimataifa, yasiyofungamana na dini yoyote, yanayofanya kazi ya kuinua hali za maisha na kutoa fursa kwa watu wanaoishi katika maeneo yenye huduma duni katika nchi zinazoendelea.

Mwakilishi mkazi wa mtandao, Amin Kurji amesema fursa za ajira zimetengenezwa, imeongeza kipato na kupunguza umaskini katika nchi za barani Afrika na Asia, huku Tanzania ikinufaika kupitia maisha ya Watanzania wanaopata huduma za lishe bora, afya, elimu na maendeleo ya uchumi.

Kurji ametoa kauli hiyo jana Jumatatu Julai 15, 2019 katika sherehe za miaka 62 ya mtukufu Aga Khan  akiwa mrithi wa 49 kwa kuzaliwa kama kiongozi wa kiroho wa madhehebu ya waislamu wa Shia Ismaili Ulimweguni.

Maadhimisho hayo yamefanyika ikiwa ni sehemu ya kutambua kazi za Mtukufu Aga Khan aliyejitoa maisha yake katika kusaidia maendeleo ya mamilioni ya watanzania kwa zaidi ya karne sasa. 

Akitaja baadhi ya mafanikio yaliyofanyika kupitia mashirika hayo, Kurji amesema Chuo Kikuu cha Aga Khan kwa sasa kinatoa Shahada ya Uzamivu ya Elimu na kozi fupi za astashahada, stashahada ya elimu kwa walimu wa shule za msingi wenye astashahada za daraja la “A”.

 

“Tangu 2014, taasisi imetoa mafunzo kwa wanufaika zaidi ya 6,000 kupitia kozi hizi,” amesema.

Amesema katika miaka minane iliyopita, Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Aga Khan, limetoa mafunzo kwa wakulima wadogo 136,000, asilimia 46 kati yao wakiwa wanawake kwa lengo la kuongeza tija, kuwaunganisha na masoko, kujenga uwezo wa biashara ndogo, za kati 412 ili kuongeza kipato na ajira.

“Imeratibu watu 184,000, asilimia 66 kati yao wakiwa wanawake wa vijijini katika zaidi ya  vikundi 9,200 vya kuweka akiba na hivi sasa inafanya majaribio ya huduma ya kuweka akiba kijiditali kwa ajili ya upanuzi,” amesema.

Aidha, amesema tayari Hospitali ya Aga Khan imeanzisha vituo 23 vya utoaji huduma za afya na vituo vya matibabu ya awali kote Tanzania, hatua itakayowezesha uundaji wa mfumo wa kuunganisha huduma za afya katika mikoa 11 ya Tanzania.

Kurji alisema AKF kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Aga Khan, inafanya kazi na vituo vya afya vya umma 80 katika mkoa wa Mwanza ili kutekeleza mradi unaofadhiliwa na Global Affairs Canada, Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Aga Khan kwa lengo la kuboresha upatikanaji, utumiaji, ubora na uwezo wa huduma za afya ya wajawazito na watoto wachanga.

Chanzo: mwananchi.co.tz