Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtalaamu aeleza namna ya kumtambua mwanaume, mwanamke mwenye kitambi

10454 Pic+kitambi TanzaniaWeb

Sun, 1 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kuna baadhi ya viashiria katika mwili wako endapo utajichunguza na kuvibaini, basi tambua ni mnene kupita kiasi.

Ukichukua kipimo cha urefu (tape measure) ukapima tumbo huku ukikipitisha kwenye kitovu kuzunguka hadi kiunoni, kwa mwanaume mwenye zaidi ya inchi 40 utakuwa na kitambi na mwanamke atakayepata zaidi ya inchi 35 atakuwa nacho.

Mtaalamu wa afya ya jamii, Dk Ali Mzige aliyasema hayo wakati akichangia mada kwenye mjadala wa kwanza wa Mwananchi Jukwaa la Fikra uliofanyika jijini Dar es Salaam Juni 28.

“Mwanaume kuwa na inchi 40 una kitambi na kwa mwanamke ikifika nchi 35 kitambi. Sasa Muhimbili mnapandikiza figo wenzenu wanapandikiza vitambi,” alisema Dk Mzige.

“Sasa kwa mwenye tatizo kama hilo ajue kabisa ana athari ambazo zitaleta saratani, shinikizo la damu, kisukari na pia tatizo kati ya magoti na kitovu. Matatizo mengi hapo siwezi kuyasemea, lakini ndiyo yanayoathiri wanaume.”

Hata hivyo, Dk Mzige alisema watu wengi bado hawajajua namna sahihi ya kupunguza uzito.

Alisema inashauriwa kupima uzito mara kwa mara, ingawa ni vyema ikwa mara moja kwa wiki kwa kuwa uzito wa maji hubadilika kwani kwa kawaida theluthi mbili ya mwili wa binadamu ni maji endapo mtu hana kitambi.

Alisema mtu akiwa na kitambi kunakuwa na mafuta na nyama huchukua nafasi ya maji mwilini.

Dk Mzige alisema ni vyema kupunguza matumizi ya vyakula vya mafuta kwa kuwa hayatakiwi kuzidi asilimia 10 ili mwili ufanye kazi vizuri.

Alifafanua kuwa, dhamira ya kupunguza uzito iko katika ubongo wa mtu, kunywa maji vikombe viwili au glasi mbili kabla ya kula kwa kuwa humsaidia asile chakula kingi.

Alisema endapo figo zinafanya kazi vizuri, uzito utapungua.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa kabla ya kuamua kupunguza uzito ni vyema kupima figo, na kwa mwenye figo zisizofanya kazi vizuri na ini lenye kasoro hastahili kufunga kwa ajili ya kupunguza uzito. “Usiache kula chakula cha mchana ili ukonde, ni makosa. Kula vyakula vya asusa upate nguvu ya kufanya kazi, kipande cha muhogo uliochemshwa, magimbi, karanga, ndizi, matunda na mbogamboga. Kunywa au kula chakula cha asubuhi ikiwemo uji wa viazi vitamu au magimbi, vyakula vya kuchemsha ni vizuri sana kuliko kukaanga,” alisema Dk Mzige.

Alisema mtu anaweza kutumia kati ya dakika 15-20 wakati anakula, na si vyema kula kwa haraka kama anafukuzwa kwa kuwa ni vizuri kutafuna chakula ipasavyo.

Dk Mzige alisema kwa kawaida hamu ya kula iko kwenye ubongo wa mtu mwenyewe na humpa ujumbe kwamba sasa anaelekea kushiba endapo atakuwa anakula taratibu.

“Utafiti umeonyesha kuwa wanawake waliokula haraka waliongezeka uzito ukilinganisha na wale waliokula kwa muda wa dakika 15-20,” alisema mtaalamu huyo.

Dk Mzige alisema ni vyema kuweka kumbukumbu ya vyakula anavyokula mtu ili ajue nishati lishe, karoli na aina ya chakula akisisitiza kuwa gramu moja ya mafuta inampa karoli tisa, gramu moja ya sukari na chakula cha nafaka kinampa karoli nne na gramu moja ya utomwili-protini unampa kalori nne.

Hata hivyo alisema mafuta hunenepesha sana hasa nyama ya nundu na sehemu zote zenye mafuta.

“Epuka vyakula vya kusindika kama soseji, baga na chipsi mayai, chipsi kuku wa kukaanga, epuka unywaji wa soda kwani moja hukupa vijiko 10-12 vya sukari - nayo inanenepesha na ikizidi mwilini inahifadhiwa kama mafuta kwenye ini lako,” alitahadharisha.

Alisema ulaji wa mbogamboga kwa wingi na matunda haviwezi kumuongezea mtu uzito.

Dk Mzige alisema ili kupunguza uzito haraka inashauriwa mtu alale kati ya saa 6 hadi 7 kwa siku na iwapo atakosa usingizi, atasikia njaa na kukosa homoni ya kumfanya akue. “Wazee wengi hukosa usingizi kwa kuwa hawana homoni za kuwafanya wakue, hii husababisha kongosho lishindwe kutengeneza insulini ya kutosha, matokeo yake ugonjwa wa kisukari unaingia, ukilala usingizi hutakula,” alisema.

Alishauri kuwa ni vyema mtu akala saa mbili kabla ya kulala na asile mpaka akavimbewa kwani hakihitajiki chakula kingi wakati wa kulala.

Dk Nzige alisisitiza kuwa mazoezi ni muhimu kwa kuwa huongeza CD4, hupunguza lehemu na presha hushuka.

Chanzo: mwananchi.co.tz