Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtaalamu azungumzia hatari saratani ya matiti

2bc1344263d39fae4c0396a9afc47175 Mtaalamu azungumzia hatari saratani ya matiti

Mon, 14 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) iliyopo Dar es Salaam, Dk Crispin Kahesa amezungumzia kiundani hatari ya ugonjwa wa saratani ya matiti huku akibainisha kuwa, wastani wa umri wa wanawake wanaogundulika kuugua saratani hiyo, umepungua.

Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2008/2009 wanawake waliougua saratani hiyo walianzia miaka 64, lakini mwaka 2019 walianzia miaka 56. Dk Kahesa aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mwezi ujao ambao ni maalumu duniani kuhamasisha na kuelimisha kuhusu saratani.

Alisema takwimu hizo zinaonesha hali hiyo ni kiashiria cha hatari kwamba saratani hiyo imeanza kushambulia hadi wanawake wenye umri mdogo tofauti na miaka ya nyuma.

“Umri wa miaka 56 ni wastani ambao tumeupata baada ya kujumlisha data zetu. Wapo hadi wanawake wenye umri kuanzia miaka 25 ambao tumewakuta na saratani hii, hapa katika taasisi yetu,” alisema.

Dk Kahesa alisema kwa mujibu wa takwimu za taasisi ya Globalcan za 2018, zaidi ya wagonjwa 42,060 wa saratani hugundulika kila mwaka Tanzania na kati ya hao asilimia 7.2 ni wa saratani ya matiti.

“Katika uhalisia, takwimu zetu nchini zinaonesha mwaka 2018 wagonjwa wa saratani waliohudhuria hospitalini ni zaidi ya 12,215 kati ya hao 42,060 wanaokadiriwa,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk Kahesa, kati ya wagonjwa 12,215 waliokwenda hospitali, wanawake wenye saratani ya matiti walikuwa wastani wa asilimia 16 ya wagonjwa wote.

“Hapa Ocean Road ambako tunapokea wagonjwa kutoka nchi nzima, mwaka 2018/19 tuliona zaidi ya wagonjwa 7,426 kati ya hao 965 walikuwa wa saratani ya matiti ambao ni wastani wa asilimia 13,” alisema.

Alisema takwimu za ORCI zinaonesha saratani ya matiti ni tatizo kubwa ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa, baada ya saratani ya kizazi na saratani ya tezi dume.

Alisema takwimu zinaonesha kuna hatari ya wanawake 17 kwa kila wanawake 100,000 kupata saratani hiyo na kibaya zaidi, kati ya wanawake 100,000 wanawake 22 hupoteza maisha kutokana na saratani hiyo.

Dk Kahesa alisema, wataalamu wa taasisi hiyo wamejipanga kuelimisha jamii kuhusu saratani hiyo na kufanya uchunguzi wa awali ili kuwagundua mapema wagonjwa.

“Kwa kuwa tunaona wenye umri mdogo nao wanagundulika, sasa tunakusudia kuwafikia moja kwa moja, tutaanza na vyuo viwili, na hapa ORCI tunaendelea kutoa elimu na kufanya uchunguzi wa awali,” alisema.

Alisema saratani hiyo huathiri jinsi zote, lakini kwa wanaume ni kwa kiwango kidogo cha asilimia moja huku kwa wanawake ikiwa asilimia 99.

Chanzo: habarileo.co.tz