Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msongo wa mawazo huwajengea wanawake ukatili

78d57b999bbc368161a446e8adcfccf8.png Msongo wa mawazo huwajengea wanawake ukatili

Wed, 23 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MSONGO wa mawazo unaowakabili wanawake wengi umesababisha wengi wao kufanya vitendo vya ukatili vinavyosababisha hata mauaji kwa watoto huku utegemezi ukitajwa kuwa chanzo kikuu cha wanawake kukumbwa na matatizo ya msongo.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Agness Punjila, alisema hayo wakati akizungumza katika Kongamano la Kupinga Ukatili lililoandaliwa na Asasi ya Maendeleo ya Wanawake Kigoma (Kiwode) hivi karibuni.

Alisema wanawake wengi wamekuwa wakikutana na ukatili kutoka kwa wanaume wanaoishi nao kwa kuwa hawana vyanzo vya mapato vinavyowawezesha kuingiza kipato hali inayowafanya wanaume wengine kuwaona wake zao kama vitu na mizigo jambo ambalo si sahihi.

Alisema inapotokea migogoro, baadhi ya waume hunyimwa wake zao mahitaji muhimu kama chakula, hali inayowafanya wanawake hao kukabiliwa na hali ngumu ya maisha na hatimaye, kukumbwa na msongo wa mawazo.

"Suluhisho la tatizo hilo ni kwa wanawake kuanzisha miradi ya kiuchumi ambayo itawafanya kujiingizia kipato kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao muhimu, lakini pia itawasaidia kuchanganyika na wengine na kuondokana na hali hiyo,"alisema Punjila.

Mwezeshaji katika kongamano hilo, Deogratius Sowoki, alisema kuwa kwa kiasi kikubwa msongo wa mawazo unaokumba wanawake wengi unatokana na mateso wanayopata kutoka kwa waume zao, lakini wanashindwa kutoa taarifa wanapofanyiwa ukatili.

Sowoki alisema kuwa japokuwa kumekuwa na maendeleo kiasi katika utoaji wa taarifa dhidi ya ukatili wanaofanyiwa wanawake, bado wengi wanakaa kimya licha ya ukatili wanaofanyiwa na hatimaye, kufanya uamuzi wenye madhara makubwa kwao likiwemo kosa la kujiua hata kwa kujinyonga.

Mkurugenzi wa asasi ya maendeleo ya wanawake Kigoma (KIWODE), Sophia Patrick, alisema kuwa kongamano hilo limefanyika ili kuwaweka pamoja wanawake waliofanyiwa ukatili na kutambuliwa. Kongamano hilo linalenga pia kuanzisha mipango kwa wanawake kufanya shughuli za kuwaingizia kipato.

Chanzo: habarileo.co.tz