Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

"Msiwakate watoto kimeo wanaweza kupata Ukimwi"

Kimeo Mfano wa Kimeo ndani ya kinywa cha binadamu

Thu, 7 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Kitengo cha Watoto Mahututi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Yasser Said, amewataka wazazi kuacha tabia ya kuwakata kimeo watoto kwakua kuna madhara mengi yanayoweza mengi yanayoweza kumtokea mtoto ikiwemo kifo na UKIMWI.

Akizungumzia suala hilo jana Dk. Said alisema katika jamii imekuwa ni kawaida kwa wazazi au walezi kuwakata watoto wao kimeo ambacho ni kinyama kidogo kinachokaa kwenye kinywa upande wa juu.

“Kimeo kina kazi kuu ya kuzuia chakula kisipande eneo la pua la juu ili usipaaliwe, mtu anayekata kimeo ataendelea kupaaliwa tu tofauti na wale ambao hawajakatwa,” alisema.

Alisema madhara ambayo hujitokeza ni kuvuja damu kwa wingi hadi kumsababishia umauti.

“Ipo nafasi kubwa kupata maambukizi ya homa ya ini, UKIMWI na tetenasi, jamii ifahamu panapotokea tatizo la kukohoa kituo cha kwanza ni kupata ushauri wa daktari,” alishauri.

Dk. Said alitaja sababu kubwa ya watu kukata kimeo huwa ni baada ya kumwona mtoto anakohoa.

“Watoto wengi wanapokohoa wazazi wanashauriana inawezekana ni kimeo, zipo sababu nyingi zinazosababisha mtu kukohoa inawezekana ikawa pumu, Nimonia au kifua cha kawaida, ninaomba jamii ifahamu mtoto anapokohoa msikimbilie kukata kimeo wafuate ushauri wa daktari,” alishauri.

Mtaalam huyo alitaja madhara ambayo hujitokeza mtu anapokatwa kimeo na tangu mwaka huu uanze amepokea watoto watatu wote wakiwa wameshakatwa na wawili wamefariki.

Maua Juma mkazi Kiwalani Minazi Mirefu alisema yeye ni mhanga wa mtoto aliyekatwa kimeo baada ya kumwona anatapika na kukohoa alishauriwa na watu wa karibu akakatwe.

Alisema baada ya kukatwa mtoto akapata matatizo makubwa ikiwamo kutapika damu, kunya choo cheusi na hali yake ikawa mbaya.

“Nilikwenda hospitali ya jirani wakashindwa nikapewa rufaa nikaja Muhimbili walivyonipokea hali ilikuwa mbaya madaktari wamepigana mpaka hapa sasa anaendelea vuzuri. Ushauri wangu kwa jamii siyo kila kifua au kutapika ni kimeo,” alishauri.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live