Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msipuuze tahadhari kuepuka corona- Wizara

4b8afca5814726f70c19efaad7e5d203.jpeg Msipuuze tahadhari kuepuka corona- Wizara

Mon, 12 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKURUGENZI wa Kinga wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Leonard Subi ametoa mwito kwa wananchi wasipuuze kanuni za kujikinga na virusi vya corona.

Akizungumza na HabariLEO jana jijini Dar e Salaam, Dk Subi alisema ni vyema Watanzania wakatambua kuwa kupuuza maelekezo ya wataalamu wa afya kuhusu kujikinga na virusi vya corona ni kuendelea kuhatarisha maisha yao na ya wengine.

“Jambo la msingi hapa ni kwamba wimbi la tatu la corona lipo nchini, niwasihi na kuwahimiza Watanzania wote tuchukue tahadhari, tufuate maelekezo ya wataalamu wa afya ya kujikinga na corona, tuvae barakoa, tunawe mikono kwa maji tiririka na sabuni, kuepuke msongamano na kuwahi mapema hospitali unapohisi hauko vizuri,”alisema.

Dk Subi alitaka wananchi wabadili mtazamo kuhusu ugonjwa wa Covid-19 na wazingatie maelekezo ya wataalamu.

“Tuchukue tahadhari kila mmoja wetu, ukijilinda wewe utamlinda na mwingine na kama sote tutajilinda ugonjwa utadhibitiwa, tunaendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu tahadhari ya ugonjwa huu,lakini tunapopuuza tunaongeza hatari ya kuusambaza kwa wananchi wengi zaidi,”alisema.

Kuhusu chanjo, alisema serikali imejipanga kuhakikisha chanjo zinatakotumika nchini ni zenye ubora na kuwataka wote wanaotaka kupata chanjo hiyo wawe tayari kwa sababu muda si mrefu huduma hiyo itaanza kutolewa nchini.

Juzi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watot, Dk Dorothy Gwajima aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya zote nchini wazingatie, kufuata na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu miongozo ya kujikinga na kudhibiti mlipuko wa virusi vya corona wimbi la tatu.

Alisema wagonjwa wa corona nchini wameanza kuongezeka katika hospitali hivyo viongozi wa mikoa na wilaya hawana budi kuhamasisha na kuelimisha wananchi kuendelea kuchukua tahadhari.

Dk Gwajima alisema wizara hiyo itakuwa na rejesta itakayoonesha kila halmashauri imefanya vipindi vingapi hasa kwenye vyombo vya habari vya ndani kuelimisha wananchi kujikinga na maradhi hayo kwa kunawa mikono,kuvaa barakoa,kutumia vipukusi na kuepuka misongamano.

Wiki iliyopita wakati akiwa njiani kutoka Dodoma kwenda Morogoro Rais Samia Suluhu Hassan alitaja mikoa yenye wagonjwa wa corona kuwa ni Arusha, Dodoma, Mwanza na Dar es Salaam.

Alisema corona ipo na lazima wananchi wajikinge na balaa hiyo na waache kupuuza kwa kwa madhara ya kufanya hivyo ni makubwa.

“Tuchukue tahadhari tujikinge na hili gonjwa, ni balaa likianza kupukutisha linamaliza tusifike huku kama tunavyoona kwa wenzetu, tuchukue hatua,”alisema Rais Samia.

Chanzo: www.habarileo.co.tz