Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msajili Baraza la Famasi aonya wenye vyuo binafsi

2f5197578e21289fa5fa1736ac15c80b Msajili Baraza la Famasi aonya wenye vyuo binafsi

Sun, 3 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAMILIKI wa vyuo binafsi vya kada ya famasi nchini, wametakiwa wasibadilishe vyuo vikawa kama biashara, kwani serikali inatarajia kupata wataalamu watatoa huduma zinazostahili kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Msajili wa Baraza la Famasi, Elizabeth Shekalaghe ofisini kwake jijini Dodoma.

Shekalaghe alisema kuwa kila mwaka idadi ya vyuo inaongezeka. Alisema hadi sasa baraza hilo limeidhinisha vyuo 52 ngazi ya cheti hadi diploma, ambavyo tayari vimesajiliwa na NACTE. Hivyo, alisema lazima kuwe na wataalamu wenye uwezo ambao wanaendana na mahitaji ya sasa.

"Kama Baraza la Famasi tunao wajibu wa kusimamia kwa umakini vyuo ili kuhakikisha ubora wa mafunzo yatolewayo iendane na mitaala na mahitaji kulingana na hali ya sasa" alisema.

Shekalaghe alisema idadi ya wataalamu wa kada ya Famasia, imekua ikiongezeka ingawa si kwa kasi kubwa.

Alisema ndani ya miaka miwili, Baraza limesajili wafamasia 2,111.

Kwa upande wa fundi dawa sanifu, Shekalaghe alisema ndani ya miaka miwili iliyopita baraza hilo limesajili wataalamu wa kada hiyo 365 na hivyo kuwa na mafundi dawa sanifu 3,040 nchini.

"Upande wa fundi dawa sanifu kwa mwaka huu tumesajili wapatao 694, kada hii bado inahitajika ili kuweza kusimamia utoaji wa dawa kwenye vituo licha ya kwamba bado wanaendelea na mafunzo ngazi ya stashahada" alisema.

Kwa upande wa usimamizi wa maduka ya dawa muhimu, Shekalaghe alisema Baraza la Famasi limekasimu baadhi ya majukumu katika ngazi ya halmashauri kwa mujibu wa sheria. Alisema wanaendelea kuendesha mafunzo kwa wakaguzi ili kuwakumbusha maadili, miiko na majukumu yao kama wafamasia na wakaguzi.

Alisema kwa mwaka mpya ujao, wamejipanga kumalizia kuwajengea uwezo wakaguzi hao nchi nzima na kazi hiyo itakuwa endelevu.

Chanzo: habarileo.co.tz