Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mradi wa kupambana na udumavu unaandaliwa

F8eb37a984e864ba99bdb62e4b5401db Mradi wa kupambana na udumavu unaandaliwa

Tue, 8 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UONGEZAJI wa virutubisho kwenye chakula cha mtoto katika ngazi ya kaya, ni njia mojawapo ya kukabiliana na tatizo la upungufu wa vitamini, madini mwilini na utapiamlo hasa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Tatizo la lishe bora ambalo huchangia udumavu linawaathiri hasa watoto wenye umri kati ya miezi sita na miaka mitano. Lakini huwa na athari mbaya zaidi kwa watoto wenye umri kati ya miezi sita na miaka miwili.

Kinachotakiwa kwa wazazi majumbani ni umuhimu wa kuongeza virutubisho vilivyo katika hali ya ungaunga kwenye vyakula laini vya nyongeza katika ngazi ya kaya.

Mchanganyiko wa virubitisho uliofungashwa ndani ya pakiti unapaswa kutumika katika mlo mmoja kwa siku kwa mtoto mmoja. Huu unapaswa kuongezwa kwenye chakula na kuchanganywa vizuri kabla ya kumlisha mtoto.

Mtafiti Lishe wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Luitfrid Nnally, amebainisha haya kwenye mada yake katika mafunzo kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Morogoro yaliyolenga kuandika na kuandaa vipindi vinavyoelimisha wananchi juu ya umuhimu wa lishe.

Nnally anasema uongezaji wa virutubisho kwenye chakula cha mtoto unachangia katika kuzuia upungufu wa damu na kumkinga mtoto dhidi ya magonjwa.

Pia uongezaji wa virutubisho husaidia kuboresha ukuaji wa mwili na akili, kuongeza uwezo wa kujifunza na kuelewa.

Pamoja na hayo kuongeza virutubisho katika chakula na utoaji wa virutubisho vya nyongeza umeonesha kutoa faida kubwa za kiuchumi.

Kwa kutambua umuhimu wake Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikishirikiana na wadau wa ndani, chini ya unafadhiliwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), imezidua mradi wa kutengeneza vyakula vya nyongeza kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara hiyo, Edward Mbanga, anaeleza mradi wa kutengeneza vyakula vya nyongeza kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano unatokana na viashiria vya kuongezeka kwa idadi ya watoto waliodumaa.

Mbanga, kwenye uzinduzi wa mradi huo alimwakilisha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Anasema kuwa idadi ya watoto waliodumaa imeongezeka kutoka milioni 2.7 mwaka 2014 hadi kufikia milioni tatu mwaka 2018 kutokana na ongezeko la jumla ya idadi ya watu.

Hivyo, anasema inakadiriwa ya kwamba kwa mwaka 2020 zaidi ya watoto 440,000 walio chini ya umri wa miaka mitano watakumbwa na utapiamlo mkali licha ya kuwepo kwa viashiria vya kupungua kwa udumavu kwa watoto walio chini ya miaka tano.

Mbanga anasema ulishaji sahihi wa watoto wakiwemo watoto wachanga umekuwa chini sana, ambapo mnamo mwaka 2018, asilimia 58 ya watoto wachanga wenye umri wa miezi 0-5 ndio waliripotiwa kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kama inavyotakiwa kiafya.

Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara hiyo pia anasema kuwa asilimia 35 ya watoto wenye umri wa miezi 6-23 walipatiwa vyakula mchanganyiko kwa kiasi kidogo, wakati asilimia 30 walipata kiwango cha chini cha chakula kilichokidhi mahitaji ya mtoto.

Katika kupambana na utapiamlo, Serikali imekuwa ikitekeleza mpango mkakati wa Kitaifa wa Lishe ulioanza mwaka 2016 na unatarajia kufikia tamati 2021.

“Mpango huu umejikita katika kuhakikisha watoto, wanawake na wanaume wanapata lishe bora na kuondoa utapiamlo, ukondefu na udumavu,” anasema Mbanga.

Mbanga anasema licha ya Serikali kuweka mkakati katika kupambana na utapiamlo kwa watoto walio chini ya miaka mitano, suala la uongezaji wa virutibisho kwenye vyakula vya watoto wenye umri huo katika ngazi ya kaya ni la muhimu kutekelezwa.

“Hadi sasa hakuna uzalishaji wa kibiashara wa vyakula vya nyongeza hapa nchini na badala yake vimekuwa vikiagizwa kwa wazalishaji mbalimbali kutoka nje ya nchi,” anasema Mbanga.

Mbanga anasema mradi huo utahusisha vyakula vya nyongeza vinavyopatikana nchini ambavyo pia vitasaidia kuboresha matibabu ya utampiamlo wa kadiri na vitatoa ajira kwa Watanzania watakaozalisha vyakula hivyo.

“Mradi huu utakuwa msaada mkubwa kwa jamii kwani utengenezaji wa vyakula vya nyongeza kwa ajili ya watoto chini ya miaka mitano utasaidia kuzuia na kutibu utapiamlo wa kadiri nchini, na ni wazi vyakula vitakavyohusika ni vile ambavyo vinapatikana hapa nchini,” anasema Mbanga.

Pia anasema kuanzishwa kwa mradi huo kutaifanya Tanzania ipige hatua mbele ya kuacha kuagiza vyakula vya nyogeza kwa watoto kutoka nje ya nchi pale vitakapozalishwa kwa wingi nchini.

Mbanga anasema uzalishaji wa vyakula vya nyongeza utaziwezesha kaya kupata mahitaji yao kwa karaka na wakati, kwa ajili ya kuwawezesha watoto waliochini ya umri wa miaka mitano kupata chakula kilichoboreshwa na kinachokidhi mahitaji yao.

Anasema vyakula vya nyongeza vitaanza kuzalishwa nchini, mara baada ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kwa pamoja kutekeleza mradi huo.

Mbanga amewataja wadau wengine wa utekelezaji wa mradi huo kuwa ni Chuo Kkuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TFNC, Dk Germana Leyna, anasema mradi huo utasaidia kuongeza upatikanaji rahisi wa chakula kilichotengenezwa ndani ya nchi kikiwa salama kuweza kuwapatia watoto kwa lishe bora.

Dk Leyna anasema vyakula hivyo pia vitaweza kupatikana kwa gharama nafuu na hatua hiyo itamwezesha kila Mtanzania kumudu gharama zake na kukipata bila tatizo pale atakapokihitaji.

Pia anasema pamoja na hayo, Tanzania imeonyesha mafanikio katika jitihada za kuondoa udumavu, ukondefu na uzito uliopungua ingawa bado haijafikia malengo ya kidunia.

Mradi huo anasema utaenda sambamba na utafiti kuhusu ufanisi na kukubalika kwa vyakula hivyo na pia kutatengenezwa bidhaa za chakula kwa makundi mengine ya watu wakiwemo wanawake wajawazito na wanaonyonyesha.

Virutubisho mchanganyiko vimethibitishwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuwa ni salama kwa afya ya mtoto.

Hata hivyo, kwa mujibu wa watafiti wa lishe wa taasisi hiyo, virutubisho hivi havibadili ladha, harufu, rangi wala muonekano wa chakula.

Naye Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Andrea Pembe ambaye chuo chake ni washiriki kwenye mradi huo, anasema suala la kuagiza vyakula vya nyongeza kutoka nje ya nchi kamwe halikubaliki.

Profesa Pembe anaamini kwamba endapo mradi huo utatekelezwa kama ulivyopangwa, utasaidia kupunguza matatizo ya utapiamlo na udumavu kwa kiasi kikubwa kwa watoto waliochini ya umri wa miaka mitano nchini.

Kwa upande, Naibu wa Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) upande wa Taaluma, Profesa Maulid Mwatawala, anasema chuo chao kitashirikiana na Serikali katika kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.

Profesa Mwatawala, anasema katika mradi huo, SUA kupitia Idara ya Teknolojia ya Chakula, Lishe na Sayansi za Walaji inatarajiwa kutengeneza vyakula hivyo vya nyongeza kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Naye Juliana Muiluri, kwa niaba ya Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani hapa nchini anasema WFP iitahakikisha mradi huo unafanikiwa.

Anasema endapo mradi huo utafanyika kama ulivyokusudiwa basi utaweza kuitangaza Tanzania kwa kiasi kikubwa katika mapambano dhidi ya utapiamlo na udumavu.

Chanzo: habarileo.co.tz