Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mradi wa Pet CT-Scan wafikia asilimia 80

PET SCAN Mradi wa Pet CT-Scan wafikia asilimia 80

Sun, 20 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mradi wa ujenzi wa mashine ya kisasa ya teknolojia ya matibabu ya mionzi ya kupima saratani mwilini ‘Positron Emission Tomography-Computerized Tomography Scan (PET/CT Scan)’ umekamilika kwa asilimia 80.

Mashine hiyo itasaidia kuweza kugundua saratani mapema zaidi kwa kuweza kuona chembechembe za saratani hata kabla uvimbe haujajitokeza na pia kusaidia kuangalia matokeo ya tiba saratani kuhakiki kama imepona.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Februari 20, 2022 na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilipotembelea Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kwa lengo la kuangalia maendeleo ya mradi huo.

“Ujenzi wa huu mradi kwa sasa umekamilika kwa asilimia 80 hivyo tupo ukingoni kukamilisha mradi huu ili tuanze kutoa huduma kwa Watanzania,” amesema Dk Mollel.

Kabla ya kutembelea mradi huo Mwenyekiti wa kamati hiyo, Stanslaus Nyongo amesema huo mradi wa kimkakati.

Advertisement “Tulifika hapa wakati ujenzi ndio unaanza na tuliomba inapofika asilimia 80 na ujenzi wa mradi huu tuweze kufika na nilidhani ni mbali sana kumbe tumekaa wiki kadhaa mmeshafikia hatua hiyo.

“Kamati tunaipongeza Serikali kwa uwekezaji huu ni mkubwa na wa kimkakati unakwenda kuwakomboa wananchi.

“Kupima saratani katika hatua za awali kabisa ni mkombozi kwa taifa hili. Tunampongeza Rais Samia kwa kuweka fedha na wataalamu kwa usimamizi mzuri na tunaamini kazi ni nzuri na tutatoa mapendekezo pamoja na maoni baada ya kuona,” amesema Nyongo.

Akitoa maelezo ya mradi huo kabla ya kuanza ukaguzi, Msimamizi wa mradi huo, Injinia Reginald Matola amesema mradi huo kuna washirika watatu ikiwemo kampuni ya ujenzi kutoka Ujerumani.

Amesema mradi huo uliogharimu Sh18.2 bilioni michoro yote imesanifiwa na Ujerumani.

“Jengo hili lina urefu wa mita za mraba 1204, ndani kuna sehemu za mashine mbili za CT scan na kiwanda cha kuzalisha mionzi dawa , maabara kubwa mbili, vyumba vitano vya wagonjwa vya maandalizi na maeneo mengine,” amesema Injinia Matola.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live