Morogoro. Timu ya watumishi nane katika sekta ya afya mkoani Morogoro imeondolewa kutokana na kushuka kwa huduma za kitabibu katika halmashauri akiwemo mganga mkuu wa mkoa huo Dk Frank Jacob.
Katibu tawala mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari akizungumza na waandishi wa habari jana Juni 3,2019 katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Morogoro amesema ofisi yake kwa kushirikiana na Serikali Kuu imefikia uamuzi wa kufanya mabadiliko katika uongozi kwa sekta hiyo ya afya kwa kuondoa timu ya watumishi hao.
Tandari alisema mabadiliko hayo ni kutokana na huduma za kitabibu katika halmashauri kushuka ikiwa ni pamoja na baadhi ya hospitali na vituo vya afya madaktari kwa siku za sikukuu na mwikiendi kutofika kuangalia wagonjwa.
Alisema uamuzi huo umekuja baada ya kubainika kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo ya rushwa na kutowasikiliza wagonjwa.
“Tutabadilisha mganga mkuu wa mkoa, Muuguzi mkuu wa mkoa, mganga mkuu wa meno na wataletwa wapya pamoja na wasimamizi wa idara mbalimbali zilizopo katika timu ya mkoa,” alisema Tandari.
Pia alisema kama mkoa umeamua kuwaleta watumishi wapya na kuwaondoa waliokuwepo nia ikiwa ni kuimarisha utendaji na watakaoletwa watapewa miongozo na kuisimamia vyema.
Pia Soma
- Mrembo wa dunia aiahidi makubwa Tanzania
- TPSF, Trademark East Africa wajazwa mamilioni ya kufadhili mikutano
- Naibu Waziri Mgumba ataka vijiji vitenge ardhi kuajiri vijana
“Mamlaka zilizofanya hivyo zisisite pindi zitakapoona kwamba kuna masuala ambayo yanajirudia kati ya hawa walioondolewa na hii italeta uwajibikaji, hata waliondolewa wakafanye kazi kwa maelekezo yanayotakiwa,” alisema.