Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moi yampa mguu wa bandia Kayuni

50121 Moi+pic

Wed, 3 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Mbeya. Lucas Kayuni (52) aliyekatwa mguu wa kulia baada ya kupigwa risasi ameanza kupata wasamaria wema kumsaidia kuendesha maisha.

Gazeti hili lilichapisha mahojiano na Kayuni juzi na akasema hataki kuwa ombaomba licha ya ndugu zake kuwa tayari kumsaidia, badala yake ataendelea kufanya kazi kwa bidii bila kuomba watu.

Jana, Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi), ilisema iko tayari kumpatia mguu bandia mkazi huyo wa Mtaa wa Ilumbila jijini Mbeya.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohamed Said alitoa Sh100,000 ili kumwezesha kupata mahitaji mbalimbali. Kayuni alikatwa mguu Januari 8, 1994.

Akizungumza na Mwananchi jana, ofisa uhusiano wa Moi, Patrick Mvungi alisema mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk Respicius Boniface ametoa msaada wa mguu bandia kwa Kayuni ili kumwezesha kufanya shughuli zake za shamba.

“Moi iko tayari kumpa huo mguu kama mchango wake, anatakiwa kufika siku yoyote kuanzia sasa ili afanyiwe vipimo na wataalamu wetu ili wajue ni mguu wa aina gani hasa unamfaa,” alisema Mvungi akiongeza kuwa mguu bandia hugharimu kati ya Sh900,00 hadi 2.5 milioni.

Alisema baada ya kufanyiwa vipimo hivyo ataondoka, lakini atatakiwa kurudi kufundishwa namna ya kuutumia.

Wakati Moi ikitoa msaada huo, Kayuni alisema hana uwezo wa kufika Dar es Salaam kutokana na kutokuwa na fedha na kwamba hata Dar es Salaam hana ndugu ambako anaweza kufikia.

“Ninashukuru sana gazeti Mwananchi kuwa karibu na mimi. Uwezo wa kufika Dar es Salaam kwa kweli sina, ikizingatiwa kipindi hiki ndio tupo shambani, sina fedha wala chochote ninachoweza kuuza ili nipate nauli,” alisema.

Soma zaidi>> VIDEO: Risasi ilivyompa ulemavu wa mguu Kayuni



Chanzo: mwananchi.co.tz