Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moi yaanzisha kliniki inayotembea

Moipic Moi yaanzisha kliniki inayotembea

Sat, 26 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Taasisi ya Mifupa (MOI) imeanzisha huduma ya kliniki inayotembea kwenye mitaa na vituo vya afya kwa lengo la kukabiliana na msongamano wa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu.

Takwimu zinaonyesha kuwa kwa siku moja taasisi hiyo inahudumia wagonjwa kati ya 700 hadi 800 kwa siku moja ikijumuisha wagonjwa wa kliniki na wanaofuata matibabu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ajali.

Kuanzishwa kwa kliniki hiyo kunalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kibingwa zinazotolewa na Moi bila kulazimika kufunga safari kufuata matibabu hayo Muhimbili.

Kliniki hiyo itakwenda sambamba na mafunzo kwa watoa huduma wa hospitali na vituo vya afya yatakapofanyika matibabu hayo ili kuwawezesha kutoa huduma hizo kupunguza watu kukimbilia kwenye taasisi hiyo kwa ajili ya matibabu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kliniki inayotembea uliofanyika Mbagala jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa tiba wa MOI, Dk Samwel Swai amesema kwa hali ilivyo sasa taasisi hiyo ya mifupa inazidiwa na idadi ya wagonjwa hivyo kuna umuhimu wa kliniki hizo na wataalamu katika vituo vya afya kuwezeshwa kutoa huduma ndogo ndogo zinazohusu mifupa, migongo na mishipa ya fahamu.

“Tunataka siku za usoni huduma zote za kibingwa zinazohusu mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu zitolewe kwenye hospitali za wilaya na vituo vya afya halafu wenye uhitaji wa matibabu ya kibobezi ndiyo waje MOI, hii itasaidia kupunguza msongamano.

Pili, kwa kusogea karibu zaidi ya wananchi madaktari wataweza kuwapata hata wale wagonjwa ambao hawajaamua kwenda hospitali na hawajui kama wana matatizo yanayotibika, mfano unaweza kukuta mtoto amezaliwa na kibyongo yupo tu nyumbani kumbe angepelekwa hospitali angepatiwa matibabu ya tatizo lake,” amesema Dk Swai.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo ameishukuru taasisi hiyo kwa kuipeleka kliniki hiyo kwa mara ya kwanza kwenye wilaya anayoiongoza kwakuwa kuna uhitaji mkubwa wa matibabu.

“Wananchi wengi wana mahitaji ya huduma za afya, kama hapa inavyoonekana wamejitokeza kwa wingi ili kuitumia fursa hii ya kliniki inayotembea kupata huduma zinazotolewa na MOI,”amesema Jokate.

Mkazi wa Mbagala Said Likwenya amesema kliniki hiyo itawawezesha wasiokuwa na uwezo wa kufika kwenye taasisi hiyo kupata huduma kwa urahisi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live