Dar es Salaam. Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi) imesaini mkataba wa ushirikiano na hospitali ya kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking cha Beijing nchini China katika tiba, utafiti na mafunzo.
Mkataba huo umesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Dk Respicious Boniface pamoja na Rais wa hospitali ya kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking Ms, Hongxia Yu.
Taarifa iliyotolewa na Moi leo Ijumaa Agosti 17, 2018 inaeleza kuwa katika mkataba huo taasisi itanufaika katika kuboresha huduma za kibingwa za daraja la juu katika upasuaji wa mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu.
Hafla ya kusaini mkataba huo imeshuhudiwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ,Ummy Mwalimu pamoja na Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhamad Kambi.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya waziri Ummy ambaye yuko kwenye ziara ya kikazi nchini China kufanya kikao na hiyo kuhusiana na ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika kuboresha huduma za tiba za kibingwa hapa nchini.
Hospitali hiyo yenye uzoefu mkubwa katika matibabu ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu ambapo ina vitanda 1800 vya kulaza wagonjwa, ICU vitanda 171, vyumba vya upasuaji 48 ikuhudumia wagonjwa zaidi ya 14.7 milioni kwa mwaka.