Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moi kufanya upasuaji wa ubongo wa kihistoria

25548 PIC+MOI TanzaniaWeb

Tue, 6 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wataalamu wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Weil Cornel cha Marekani, kesho Jumanne Novemba 6, 2018 watafanya upasuaji wa kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo (Celebral aneurysm).

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Novemba 5, 2018 na Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Dk Respicious Boniface wakati wa kongamano la tano kimataifa la mafunzo ya madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu linalofanyika kwa siku tano.

Amesema kongamano hilo la tano, limehudhuriwa na zaidi ya madaktari 100 kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Ethiopia, Malawi, Namibia na nchi nyingine za Afrika, mafunzo yatatolewa na madaktari bingwa wanane wazalendo kutoka Moi na wengine 15 kutoka Marekani na Ulaya.

Dk Respicious Boniface amesema mafunzo hayo yameratibiwa na Moi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Weil Cornel cha New York Marekani ambapo hii ni mara ya tano kufanyika.

“Mafunzo ya mwaka huu yatakuwa ya kipekee zaidi kwani wataalamu wetu watajifunza jinsi ya kufanya upasuaji wa kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo (Celebral aneurysm) kwa mara ya kwanza nchini, kabla ya hapo wagonjwa walilazimika kwenda nje ya nchi kwa gharama kubwa,”  amesema Dk Boniface

Dk Boniface amesema  gharama za upasuaji huu nje ya nchi ni zaidi ya Sh60 milioni na hapa nchini haitazidi Sh10 milioni hivyo kuanza kwa huduma hii kutaokoa fedha nyingi za Serikali na tayari Serikali imeshanunua darubini maalum ya kufanyia upasuaji huu mkubwa.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu wa Chuo Kikuu cha Weil Cornel, Profesa Roger Hartl amesema ni heshima kubwa kufika Tanzania kwa mara nyingine, pia kupata fursa ya kubadilishana uzoefu na madaktari wa Tanzania na nchi nyingine duniani.

“Pamoja na mafunzo ya nadharia tutafanya upasuaji kwa pamoja kwa njia za kisasa, hili ndilo lengo letu hasa la kuja hapa.”

“Tunataka wenzetu wa Moi na madaktari walio mafunzoni waweze kutoa huduma hizo kwa weledi mkubwa, tumekuwa tukifanya hivi kwa muda sasa na tunaona wanakwenda vizuri hii inatia faraja sana,” amesema Profesa Hartl.

Amesema mafunzo ya mwaka huu yanalenga kuwajengea uwezo washiriki ili waweze kutumia teknolojia ya kisasa ya matibabu ya ubongo na mgongo na kuwapa mbinu mpya za upasuaji hususani kwa mgonjwa aliyeumia kwenye eneo la mfumo wa fahamu hususani kwenye ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu iliyoharibika.

Chanzo: mwananchi.co.tz