Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mloganzila yamaliza adha ya watu kusimama foleni juani

34773 Pic+mloganzila Tanzania Web Photo

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kama uliwahi kufika Hospitali ya Mloganzila na kukutana na adha ya kusimama juani kusubiri kibali cha kuingia kuona mgonjwa, ondoa shaka kwani mambo yamebadilika.

Pia ni hivi, ule utaratibu wa kuweka vikapu, chupa za chai na kusimama msururu mrefu kusubiri askari aliyekuwa anatoa kadi za kuingilia haupo, na kwa sasa watu wanakaa kwenye eneo maalumu lililoandaliwa.

Vilevile, askari ndiye ana jukumu la kuwafuata watu walipokaa na kugawa kadi zinazotumika kuingilia lango kuu la jengo la hospitali hiyo.

Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni wiki kadhaa tangu Mwananchi lilipoandika juu ya utaratibu mbovu uliokuwa ukitumika kwa watu wanaokwenda kuona wagonjwa hospitalini hapo.

Awali ilikuwa ni lazima kujipanga katika foleni ndefu, lakini watu walifikia hatua ya kukwepa jua kwa kulazimika kupanga foleni ya vikapu, chupa za chai na mifuko ya vyakula katika nafasi zao za foleni kisha kukaa pembeni kusubiri askari mgawa kadi afike.

Mbaya zaidi ilikuwa ikimlazimu askari kusitisha ugawaji wa kadi pale zilipokuwa zinamwishia mkononi na kurudi kwenye lango kuu kuzikusanya kisha kuendelea na ugawaji.

Kwa sasa mambo ni tofauti kwani kadi hizo zimeongezeka maradufu hali inayofanya kusiwe na usumbufu wa kusubiri muda mrefu.

Juzi, ilipotimu saa 9:57 jioni Mwananchi lilishuhudia askari akiwasili eneo ambalo watu walikuwa wamekaa wakisubiri muda wa kuona wagonjwa huku akiwa ameshika mfuko uliosheheni kadi.

Bila kupoteza muda alianza kuzigawa kadi hizo kwa kumfuata kila mtu mahali alipokaa na waliopata moja kwa moja walielekea wodini.

Kadi zilipoisha kwenye mfuko askari mwingine kutoka lango kuu la kuingilia wodini alikuja akiwa nazo nyingi na kuendelea kuzigawa.

Kwa utaratibu huo, hakuna mtu anayesimama juani na eneo lililotengenezwa kwa ajili ya kupumzikia wanaosubiri kuona wagonjwa linatumika kama inavyotakiwa.

Akizungumzia suala hilo, mkazi wa Mwananyamala, Amina Kizingiti alivutiwa na utaratibu huo mpya akisema hivyo ndivyo ilipaswa kufanyika siku nyingi.

“Ila yafanyike maboresho zaidi hivi vibanda viongezwe au viti viongezwe maana wakati mwingine kukaa chini haieleti picha nzuri,” alisema.

Emmanuel Machanga alieleza kuwa changamoto iliyobaki ni uhaba wa maeneo ya kukaa. “Upungufu uliobaki ni mdogomdogo, zile sehemu za kukaa ni chache na kwa kuwa sasa hivi hakuna kusimama basi wengine wanalazimika kukaa chini kusubiri askari atoe kibali,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz