Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkurugenzi wa Tiba: Hii hapa mikakati yetu kuikabili corona

Dk. Leonard Subi Mkurugenzi wa Tiba: Hii hapa mikakati yetu kuikabili corona

Thu, 8 Jul 2021 Chanzo: ippmedia.com

Mnamo Juni 28 mwaka huu, Rais Samia aliweka wazi tayari kuwapo wastani wa wagonjwa 100 na kati yao, 70 walikuwa wanapumua kwa msaada wa mashine.

Kutokana na hatua hiyo, Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Leonard Subi, wao wakiwa wenye dhamana, katika mazungumzo na Nipashe, amefafanua hatua wanazochukua kuirejesha nchi kwenye ahueni. Kwa namna gani?

MAABARA ZA UPIMAJI

Dk. Subi anasema suala muhimu wanalolifanya ni kuwa na maabara za kutosha za upimaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema walianza na maabara moja baadaye wakaongeza zingine lakini na sasa kuna vituo vingi katika kila mkoa vya kukusanyia sampuli ili kusafirisha kwenda kupima.

“Wizara tumesema tunataka kupanua wigo wa kuongeza maabara. Hasa badala ya kuwa nazo maabara mbili za Arusha na Dar es Salaam, tunataka tuongeze maabara Kanda ya Ziwa moja ya upimaji pia Dodoma, na tumeshafanya tathmini ya awali na utaratibu unaendelea kuhakikisha tunakuwa na maabara," anasema.

Dk. Subi anasema lengo la kuwa na maabara za kutosha ni kuhakikisha wanasogeza huduma karibu na wananchi ili kupunguza adha ya kusafirisha sampuli umbali mrefu.

Anasema tayari walishaanzisha upimaji katika viwanja vya ndege, mipaka yote kwa lengo la kuimarisha na utambuzi na wanapima vinasaba vya virusi vya corona ili kuona ubadilikaji wake.

Anasisitiza kuwa eneo hilo wamelipa kipaumbele kikubwa katika kuhakikisha watu wanapata huduma stahiki na kwa wakati.

Kadhalika, anasema wanahakikisha kusiwe na ucheleweshaji wa majibu na wananchi wapate huduma stahiki katika eneo la maabara na upatikanaji wa maji na sabuni za kunawia uwe wa uhakika katika maeneo hayo.

Anasema pia wameweka mkakati wa kutoa msaada wa saikolojia kwa ndugu wa watu waliopoteza maisha kutokana na janga hilo ili wasahau na kuendelea na maisha mengine.

Dk. Subi anasema huduma hiyo itatolewa katika ngazi zote na wanawashirikisha viongozi wa dini katika kuhakikisha wanapata elimu ya kutosha.

URATIBU

Mtaalamu huyo wa afya anasema uratibu unaendelea pamoja na utafutaji wa rasilimali na tayari serikali na wadau mbalimbali wameendelea kujitokeza kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Anasema wananchi na watu binafsi na mashirika ya kimataifa bado wanaendelea kujumuika na wizara katika kuhakikisha wanadhibiti ugonjwa huo nchini.

Anasema wanaendelea na uratibu wa kuimarisha wataalamu wa ndani wakiwamo watumishi wa afya ili kuhakikisha wako imara katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

“Hili linaenda sambamba na kuhakikisha katika maeneo yote muhimu kwenye vituo vyetu vya huduma kwenye maeneo ya mipakani tunakuwa na rasilimali ya kutosha katika kukabiliana na ugonjwa huu.

"Lakini tunashukuru kwamba uratibu huu siyo katika ngazi ya taifa tu pia katika ngazi ya mikoa wameandaa mipango mikakati ambayo inaiandaa kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huu,” anasema.

UDHIBITI WA MIPAKA

Anasema pia wameimarisha ufuatiliaji na udhibiti wa ugonjwa huo katika maeneo yote, yakiwamo ya mipakani kwa kuanzisha huduma ya upimaji wa corona.

“Sisi tunachokifanya katika maeneo ya mipakani hatupimi tu corona, tunapima na maradhi mengine ili kuhakikisha wanakuwa salama.

"Tunapokuta na maradhi, tunawaweka karantini kwa siku 14 kuhakikisha wanakuwa sawa kabla ya kwenda kujichanganya na wengine," anafafanua.

Anasema wamekuwa na utaratibu wa kuelimisha umma kupitia mitandao ya kijamii, runinga na nyumba kwa nyumba katika mitaa ili kuelewa na kutokuwa na hofu ya aina yoyote.

“Tunapoenda kutembea nyumba kwa nyumba, tuwaambia kabisa wasipaniki kwa sababu ugonjwa huu umekuwapo kwa muda sasa, lakini tunawaomba sana wananchi wasiupuuze kwa sababu corona ni ugonjwa na tumeshuhudia vifo vikitokea," anasema.

Dk. Subi anasema wanahimiza wananchi wachukue tahadhari na kufuata hatua zote za kujikinga kama kuvaa barakoa kwa usahihi katika maeneo ya mikusanyiko.

Anasema pia wanawahimiza watu kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi tiririka na sabuni au vipukusi.

Anasema wanasisitiza watu kunawa mikono kwa sababu watu walirudi nyuma hivyo wanapaswa kuendelea na utaratibu huo.

“Tunasema kwamba ni vizuri na kusisitiza sana maeneo yote ya umma na binafsi katika makanisa na misikiti watu watumie vipukusi, lazima tuhakikishe utamaduni wa kimila unazingatiwa, unaweza kukuta mtu ameshika meza mwingine akashika wakaambukizana," anasema.

MAKUNDI MAALUM

Dk. Subi anasema wanatoa elimu kwa watu wenye magonjwa sugu kama shinikizo la damu, moyo na wazee ambao wapo katika hatari ya kupata maambukizi.

“Na kwa bahati mbaya sasa hivi aina mpya ya virusi vya corona inaathiri watu wa rika zote, hata wa umri chini ya miaka 60,” anasema.

VIKWAZO

Dk. Subi anabainisha vikwazo katika kukabiliana na ugonjwa huo ikiwamo watu kulalamika kuwa chanjo ni mbaya ilhali dunia inaendelea kupata chanjo.

Anasema hadi sasa, kupitia WHO, watu bilioni moja wameshachanjwa na maeneo mengine wanaendelea kutoa chanjo kwa ufanisi mkubwa na watu wanaendelea vyema na majukumu yao.

Anasema kwa Afrika uchanjaji uliofanyika ni mdogo, ukiwa chini ya asilimia mbili, idadi ambayo ni sawa na kwamba bara halijachanja watu wake.

“Na ndiyo maana hapa tunasema kama nchi ni vizuri tukasema tunaanza kuimarisha uzalishaji wa chanjo ndani ya Afrika.

"Tuzalishe wenyewe, hili ni jambo la msingi, tumeona mataifa makubwa pia wamechukua chanjo karibia mataifa 10, mataifa mbalimbali duniani yamechukua asilimia 10 na mengine kama 10 tu na mengine, zimekuja kwa hiyo unaweza kuona kuna suala la tatizo la kiuchumi,” anafafanua.

Dk. Subi anasema Waafrika wanapaswa kuendelea kuungana ili kujenga teknolojia imara na nzuri ambayo pia itasaidia nchi za Afrika kujitegemea.

Anasisitiza kuendelea kuelimisha wananchi kuwa Tanzania siyo wageni katika kutoa chanjo, wakianza tangu mwaka 1970 kwa kutoa chanjo kama polio na surua.

“Sasa chanjo hii ya corona watu wanasema 'kwa nini imefanyika haraka haraka?' Siyo chanjo ya kwanza kutolewa haraka haraka, duniani zipo chanjo zingine ambazo tunaweza kutengeneza na kuanza kutolewa zikaleta matunda, kwa hiyo ipo haja ya wananchi kuelimishwa," anasema.

Dk. Subi anasema kikwazo ni upatikanaji wa rasilimali kama vifaa tiba katika hospitali zote nchini.

Anasema wanahitajika wataalamu wa kutosha, vyumba maalum vya wagonjwa mahututi, vitanda na upatikanaji wa gesi tiba.

Anarejea kuwa hivi karibuni Waziri wa Afya, alizindua mitambo saba mipya ya kuzalisha Oksijeni ambayo kila mmoja una uwezo wa kuzalisha mitungi 200 kwa siku.

MIONGOZO

Dk. Subi anasema serikali ilitengeneza miongozo katika wimbi la kwanza na la pili, hivyo wanaendelea kuipitia ili kuhimiza utekelezaji wake.

Anasema wanataka kuweka miongozo kwenye shule, michezo, viwanja vya ndege na mahali penye mikusanyiko ili watu waifuate wakati wa kutekeleza shughuli zao.

Anaitaka jamii kutopuuza ugonjwa huo, bali kuzingatia elimu inayotolewa na wataalamu wa afya kuachana na habari zisizo sahihi za kwenye mitandao na kama kuna mwenye tatizo, apige simu kwa namba 199 ili kupata msaada.

*Imeandaliwa na Mary Geofrey, Renatha Msungu na Edwin Mosha (TURDACO)

Chanzo: ippmedia.com