Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa iliyopo Dodoma Dkt. Alphonce Chandika amekiri kupokea simu sio chini ya nne kati ya nyingi zinazopigwa kutoka kwa Vijana wanaohitaji kuuza figo zao katika Hospitali hiyo.
Dkt. Chandika amesisitiza kuwa sheria za nchi haziruhusu kuuza viungo vya Binadamu “Wapo vijana wanapiga simu mimi binafsi nimepigiwa na vijana si chini ya wanne baada ya kupata namba yangu nikijua wanauliza huduma za hapa Hospitali kumbe wanataka wauze hivyo tukaona ni vema tutumie wasaa huu kuelimisha Jamii kuwa sheria za nchi haziruhusu biashara za viungo vya Binadamu na kufanya hivyo ni kosa”
Dkt.Chandika amesema hilo leo March 13,2023 Jijini Dodoma kwenye maadhimisho ya mafanikio ya miaka mitano ya upandikizaji figo katika Hospitali hiyo wa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma na Tokushukai Group kutoka Japan.
Amesema kwa kipindi hicho cha miaka mitano Watanzania 33 wamefanikiwa kupandikizwa figo kati ya hao 22 walipandikizwa na Madaktari wa kitanzania.