Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkemia Mkuu kuwa na kanzidata ya vinasaba

2918f4369f94f5e3d505d9233cd1bb2a Mkemia Mkuu kuwa na kanzidata ya vinasaba

Mon, 31 Jan 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ipo mbioni kuanzisha kanzidata ya vinasaba ya taifa kwa Watanzania ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa zikiwamo za uhalifu.

Hayo yalisemwa jijini hapa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko alipotembelea mabamba ya Maonyesho ya Wiki ya Sheria, ambapo alisema kwa sasa wapo katika mchakato huo na tayari wamempata mshauri mwelekezi wa kufanya tathimini.

"Mamalaka yetu imepewa kisheria jukumu la kuratibu na kuanzisha kanzidata ya vinasaba ya taifa na kwa sasa tuko kwenye hatua za mwanzo ndio tumempata mkandarasi wa wa kufanya upembuzi yakinifu kwa kushirikiana na wataalamu wa mamlaka ili tujenge mfumo huo," alisema.

Hata hivyo, Dk Mafumiko hakusema ni lini wataanza au wataanza na kundi gani la Watanzania kutokana na kuwa jambo hilo linahitaji umakini mkubwa ili liweze kuleta ufanishi kwa kinachotarajiwa.

Alisema mchakato huo kwa sasa upo kwa mkandarasi ambaye kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali wamefikia hatua za awali za kufanya upembuzi yakinifu kuhusu teknolojia hiyo.

Dk Mafumiko alisema endapo uanzishwaji wa kanzidata utafanikiwa, itasaidia kurahisisha utoaji taarifa za vinasaba vya wazazi endapo kutatokea migogoro kwenye familia bila wahusika kupima upya au kutumia muda wao kukutana kwa ajili ya kipimo hicho.

“Hii pia tasaidia hata kufanya utambulizi kwa mambo mengi ikiwamo ushahidi kwa vyombo vingine vya serikali kama vile haki jinai ambavyo vimekuwa vikihitaji kupata vipimo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali," alisema.

Hata hivyo, Dk Mafumiko alisema haitakuwa kazi rahisi kuwafikia Watanzania wote kwa wakati mmoja na kutolea mfano nchi zilizoendelea kama Marekani ambazo mpaka sasa hazijafanikiwa kuwafikia wananchi wake wote, hivyo kwa Tanzania huenda ikaanza na makundi maalumu.

"Siwezi kusema ni leo au kesho kwamba tunaanza na wala kuanza na kundi lipi hapana, tukumbuke waliotutangulia kama Marekani hawajafanikiwa kwa watu wote, lakini tunasubiri ushauri kutoka kwa mtu aliyepewa kazi hiyo atuambie tunaanza na makundi gani au kanda zipi," alisema.

Kuhusu uvumi wa gharama ya kupata majibu ya upimaji wa vinasaba kwamba ni kubwa, Dk Mafumiko alisema hakuna ukweli wowote katika jambo hilo kwani sehemu kubwa ya gharama zake zimebebwa na serikali, hivyo wananchi wanatozwa Sh 100,000 kwa sampuli moja.

"Mfano unapotaka kujua mahusiano ya baba, mama na mtoto basi gharama yake itakuwa ni Sh 300,000 kwa maana ya Sh 100,000 kwa sampuli moja na si vinginevyo." “Endapo Serikali isingebeba gharama basi kutokana na ghamana za vitendanishi zingekuwa Sh 700,000 mpaka 800,000.”

Akiwa kwenye Banda la Jeshi la Polisi, alihimiza ushirika wa karibu na jeshi hilo katika kuwahudumia wananchi kwenye majukumu yanayowaunganisha kisheria.

Kaimu Meneja wa Maabara ya Sayansi Jinai na Sumu, Kagera Ng'weshemi alisema ofisi hiyo imeunda mfumo (LIMS) wa kuunganisha taasisi zote zinazohusika na haki jinai ambazo zitakuwa na uwezo wa kuona moja kwa moja uchunguzi wa jalada la sampuli husika ulipofikia.

Alisema mfumo huo utawarahisishia wadau kuona uchunguzi wa jalada la sampuli zao kama ni Jeshi la Polisi, Mahakama au wadau wengine kama uchunguzi umekamilika au upo kwenye hatua ipi.

Alisema mfumo huo utaonesha sehemu ya shahidi kuitwa na mahakama ambapo itasaidia kuona kaitwa na mahakama ipi, muda upi ili kuepuka mkanganyiko wa taasisi nyingne kumuhitaji kwa muda ambao yupo eneo jingine.

Ng'wesheni alisema mpaka sasa mfumo huo umesimikwa katika maabara zote sita ambazo zitatoa ushahidi wa kitaalamu kwa majalada wanayoyachunguza kupitia njia ya kimtandao, lengo likiwa ni kuokoa gharama za watumishi kupeleka majibu ya uchunguzi kwenye mahakama mbalimbali nchini.

Chanzo: www.habarileo.co.tz