Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mitandao ya kijamii chanzo uuzaji usio halali maziwa ya kopo

Maziwa Toto.png Chanzo cha Picha ni nuktatz.com

Mon, 2 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kampuni zinazotengeneza maziwa ya watoto ya unga zinalipa majukwaa ya mitandao ya kijamii na watu wenye ushawiwishi ili kuweza kuwafikia wajawazito na akina mama kama mbinu mojawapo ya kuuza bidhaa zao, jambo linaloathiri unyonyeshaji watoto maziwa ya mama.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa harakati hizo zinafikisha ujumbe kwa wanawake duniani katika kipindi chenye changamoto zaidi kwenye maisha yao.

​Taarifa ya WHO iliyotolewa Aprili 29, 2022 jijini Geneva, Uswisi imesema kuwa sekta hiyo ya utengenezaji wa maziwa ya watoto ina thamani ya dola bilioni 55 (Sh127.8 trilioni) na sasa inatumia mbinu za masoko mtandaoni za kumlenga mama mzazi na ujumbe mahsusi kwake yeye binafsi, mbinu ambayo inatambuliwa kuwa ni matangazo ya biashara.

Taarifa hiyo imenukuu ripoti mpya ya WHO iliyopatiwa jina “Kiwango na Athari za mbinu za masoko za kidijitali za kutangaza maziwa mbadala ya mama”, ripoti ambayo inachambua kwa kina mbinu za masoko mtandaoni zilizobuniwa kushawishi familia zenye watoto juu ya jinsi ya kulisha watoto wao wachanga.

Kupitia mbinu kama vile matumizi ya programu tumishi za simu (apps), vikundi vya mtandaoni vya kusaidia malezi au lishe ya watoto, malipo kwa watu wenye ushawishi mtandaoni, matangazo na mashindano, na majukwaa ya ushauri au huduma, kampuni za kutengeneza maziwa ya watoto zinaweza kununua taarifa za mtu na kuzitumia kuandaa ujumbe mahsusi unaolenga mjamzito au mama mzazi mwenye mtoto mchanga.

Ripoti imeweka muhtasari wa matokeo ya utafiti mpya wa taarifa milioni 4 kutoka mitandao ya kijamii kuhusu ulishaji wa watoto wachanga, taarifa zilizokusanywa kati ya mwezi Januari hadi mwezi Juni mwaka jana wa 2021. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kampeni za maziwa ya kopo zinawafikia watu mara tatu zaidi ya kampeni za maziwa ya mama, jambo ambalo wataalam wa afya wanasema linaweza kuwa na athari kwa ukuaji wa mtoto endapo hatapata maziwa ya mama kwa ukamilifu.

Taarifa hizo za mtandaoni zilifikia watu bilioni 2.47 na kupendwa, kusambazwa au kupatiwa maoni mara milioni 12.

Kampuni za maziwa hayo ya watoto ya viwandani hurusha mara 90 kwa siku katika akaunti zao za mitandaoni.

WHO inasema mbinu hii ya biashara inasababisha ongezeko la maziwa ya watoto ya viwandani na hivyo kuondoa ushawishi wa mama kumnyonyesha mtoto wake kama inavyopendekezwa na WHO.

Mkurugenzi wa lishe WHO, Dk Francesco Branca, amesema suala kwamba kampuni za kutengeneza maziwa ya watoto ya viwandani hivi sasa zinatumia mbinu za kisiri na thabiti za masoko na matangazo kuongeza mauzo yake ni jambo lisilosameheka na lazima likome.

WHO imetaka sekta ya vyakula vya watoto iache mbinu za kinyonyaji kwenye soko la maziwa ya watoto wa viwandani na imetaka serikali zilinde watoto wachanga na familia changa kwa kutunga, kufuatilia na kusimamia sheria ili kutokomeza matangazo ya maziwa ya watoto ya viwandani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live