Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Minion: Teknolojia ya kung’amua magonjwa ya mimea kwa kompyuta

46974 Pic+milion

Mon, 18 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Miongoni kwa changamoto za uzalishaji wa kilimo ni magonjwa ambayo hupunguza tija kwa mkulima, kwa kupunguza mazao na kuongeza gharama za kutibu.

Teknolojia mbalimbali zimebuniwa ili kugundua na kutibu magonjwa hayo ya mimea, lakini zimekuwa zikitumia gharama kubwa na kupoteza muda mwingi tangu kuchunguza hadi kupata dawa na kutibu.

Asha Makati ni miongoni mwa wakulima walioteswa na magonjwa ya mihogo na kiasi cha kuambulia mazao machache katika shamba lake lililopo kijiji cha Kiromo wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

Anasema licha ya kusumbuliwa na magonjwa hayo ukiwamo ugonjwa wa batobato, hakujua suluhisho, hivyo aliendelea kulima kwa mazoea.

Hata hivyo, hadithi ya magonjwa hayo ilipata dawa baada ya kutembelewa na wataalamu wa kilimo shambani kwake.

Wataalamu hao waliotoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Mikocheni Dar es Salaam (Mari), walipima mimea yake na kisha kumpa mbegu mpya ya muhogo yenye ukinzani na magonjwa.

Teknolojia ya Minion

Makati ni sehemu ya wakulima wengi wanaoteseka na magonjwa lakini, hawajui suluhisho la matatizo hayo. Lakini kwa sasa imekuja teknolojia mpya ya kung’amua magonjwa inayoitwa Kiingereza kwa jina la Minion.

Teknolojia hiyo inahusisha kifaa kidogo kinachoweza kuchukua sampuli ya seli za mmea na kuzisoma kupitia kumpyuta ili kujua ugonjwa unaosumbua mmea.

Akieleza jinsi kifaa hicho, kinavyofanya kazi, mtafiti wa kujitegemea aliyeshiriki kwenye utafiti huo, Charles Kayuki anasema tofauti na teknolojia nyingine, kifaa hicho kina wepesi wa kupata majibu ya vipimo haraka zaidi.

“Kifaa hiki kinaitwa Minion, kinatengenezwa na Oxford Nanopore Technologies ya Uingereza. Kwa kifupi Minion ni kifaa kinachohamishika. Kina uwezo wa kupima mmea na kutoa majibu hapo hapo, tofauti na teknolojia nyingine ambazo tumezoea kupima mimea na kutuma vipimo kwenye maabara za ndani na nje ya nchi ili kubaini ugonjwa,” anasema Kayuki.

Anaongeza: “Naweza kwenda shambani leo na kuchukua mmea ulioathiriwa leo na nikaanza kuanza kuchukua vipimo leo na kupata majibu hapo hapo kupitia kompyuta.”

Ukikitazama kifaa chenyewe ni kidogo tu kama flashi ambayo unaiunganisha na kompyuta ambapo kila unachokifanya utakiona kwenye kompyuta.

“Mmea ukiwa shambani na ukiwa umeshambuliwa na wadudu, unachofanya ni kuweka hiki kifaa kisha kinasoma seli za mmea. Ndani ya nyuklia ya seli moja kuna jeni zinazotoa taarifa za kuendesha au maelekezo ya kiumbe hai husikia zinazoitwa Asidi DeoksiriboNukleini (DNA). “DNA inaundwa na tabia na sehemu yake inakuwa na tabia inayoitwa jeni. Sasa teknolojia hiyo inasaidia kujua hizo tabia. Huwa zimejipanga kutegemea aina ya viumbe tofauti” anafafanua Kayuki.

Anasema kirusi cha ugonjwa kikiingia kwenye mmea (kiumbe) na chenyewe DNA yake inakuwa kwenye seli ya mmea. Ukifanya uchunguzi kwenye mmea utaona pia seli ya kirusi.

“Kwa hiyo kama kuna mmea shambani unaonyesha dalili ya ugonjwa, ukifanya ‘sequence’ utajua kuwa mmea wangu umeathirika na kirusi aina fulani ili ujue dawa za kutumia,” anasema.

Usambazaji wa teknolojia

Akizungumzia majaribio waliyofanya wilayani Bagamoyo, Kayuki anasema walitumia saa 24 kugundua shamba la mkulima lililvyoathirika.

Mbali na na Bagamoyo, anasema wameshafanya pia majaribio katika wilaya za Musoma na Butiama mkoani Mara na kugundua magonjwa mbalimbali ya mimea, huku kifaa hicho kikionyesha mafanikio makubwa.

“Kwa mfano, sasa tuna tatizo la ugonjwa wa viwavi jeshi. Mara nyingi kila aina ya mdudu anakinzana na dawa anayopuliziwa. Unapopuliza dawa ni vizuri kujua unapambana na mdudu wa aina gani.

“Kwa hiyo kwa teknolojia hii tunakwenda shambani na kuchukua vipimo na kujua aina ya mdudu anaathiriwa zaidi na dawa gani. Siyo kwamba awali hatukuchukua sampuli, lakini teknolojia hii tunafanya kwa muda mfupi zaidi. Ni teknolojia yenye uwezo wa kufanya sampuli 12 kwa wakati mmoja,” anasema.

Hata hivyo, anasema teknolojia hiyo bado haijasambazwa kwenye vituo vya utafiti na kwa wakulima. Anashauri Serikali kusaidia watafiti, angalau kila kituo kiwe na teknolojia hii.

Licha ya kutosambazwa vya kutosha, anasema Tanzania inaonekana kinara wa matumizi yake kwani tangu ilipoanza kutumika mwaka 2017, Serikali ya Tanzania ilipewa tuzo kwa kutumia teknolojia ya kugundua magonjwa kwa teknolojia hiyo.

“Wao waliotoa tuzo hii waliangalia ni jinsi gani nchi imetumia teknolojia kutatua matatizo ya watu wake. Mpaka sasa kinachotakiwa ni kuonyesha nia ya kutumia teknolojia na je kuna uwezekano wa hicho kitu kifanyika?Hata hivyo kwa kweli bado matumizi haya yako chini, hatuwezi kujisifu,” anasema Kayuki.



Chanzo: mwananchi.co.tz