Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miliki bunifu za tiba mbadala sasa kulindwa na sheria ya kimataifa

Mitishamba Miliki bunifu za tiba mbadala sasa kulindwa na sheria ya kimataifa

Tue, 27 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

akala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), umejipanga kuja na sheria ya kulinda miliki bunifu za tiba za jadi maarufu tiba mbadala.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Godfrey Nyaisa amesema hayo katika kikao cha mashauriano na wadau wa tiba hizo juzi kuhusu Sheria ya Kimataifa ya Shirika la Miliki Ubunifu (Wipo).

Nyaisa amesema wanakuja na mkakati huo kwa kuwa kuna watafiti na wataalamu ambao hubuni dawa za jadi ambazo zikilindwa na kutumika ipasavyo zinaweza kuwapatia manufaa makubwa.

"Tunatambua kuwa, Taifa letu limejaliwa rasilimali nyingi za kijenetiki zitokanazo na mimea, wanyama na ujuzi wa jadi ambavyo vina thamani ambayo wengi hawafahamu na mara nyingine rasilimali hizo kutumiwa na watu wengine pasipo kuwaletea manufaa wahusika,” amesema Nyaisa.

“Hivyo, kwa sasa tumejipanga kusaidia wabunifu waweze kulinda bunifu zao na baada ya ulinzi wafaidike na bunifu hizo, na matumizi ya rasilimali hizi yawe na faida kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa jumla."

Hata hivyo, amesema kwa muda mrefu, tiba za jadi zimesaidia kutoa kinga na tiba kwa magonjwa mengi na hilo limethibitishwa na Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya 2019 inayobainisha kuwa, takribani asilimia 79 ya Watanzania wanatumia tiba za jadi.

Akizungumzia kuhusu kikao hicho, Nyaisa amesema kimejadili namna bora nchi itakavyoweza kunufaika na sheria hiyo ya kimataifa itakapokamilika, hasa katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia.

Akizungumzia Sheria ya Kimataifa ya Wipo, Kaimu Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu wa Brela, Loy Mhando amesema ikianza kutumika itazuia matumizi ya rasilimali hizo pasipo kufichua mahali zinapopatikana na kuhakikisha jamii husika zinapata faida.

Pia, amesema wabunifu watalindwa na kupewa haki ya kipekee katika matumizi ya rasilimali hizo na majadiliano ya sheria hiyo yanatarajiwa kuzaa itifaki itakayokamilishwa Mei 2024 katika mkutano wa kidiplomasia utakaofanyika makao makuu ya Wipo Jijini Geneva, Uswisi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live