Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mikoa yenye corona yatajwa

1b3d7f776b39a3eadee3623fbbca2a67 Mikoa yenye corona yatajwa

Thu, 8 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi waendelee kuchukua tahadhari kujikinga wasiambukizwe virusi vya corona.

Alisema hayo jana katika mji mdogo wa Kibaigwa akiwa njiani kutoka Dodoma kwenda mkoani Morogoro.

“Hapa naona waliovaa barakoa ni wachache sana, nataka niwaambie tuchukue tahadhari zote dhidi ya maradhi ya corona wimbi la tatu liko nchini tayari,hakuna haja ya kuficha, tuna wagonjwa kwenye baadhi ya mikoa yetu, naombeni sana tuchukue tahadhari tujikinge na hili balaa,”alisema Rais Samia.

Rais Samia alitaja mikoa yenye wagonjwa wa Covid-19 kuwa ni Arusha, Dodoma, Mwanza na Dar es Salaam.

Alitoa mwito wananchi wasipuuze tahadhari kuepuka corona kwa kuwa madhara ya kufanya hivyo ni makubwa.

“Tuchukue tahadhari tujikinge na hili gonjwa, ni balaa likianza kupukutisha linamaliza tusifike huku kama tunavyoona kwa wenzetu, tuchukue hatua,”alisema Rais Samia.

Awali Rais Samia aliishukuru kampuni ya madini ya Barrick kwa utayari wake kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19.

Alitoa shukrani hizo jana Ikulu Dodoma alipokutana na kuzungumza na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Barrick Gold, Mark Bristow.

Rais Samia alimhakikishia Bristow kuwa serikali itaendelea kushirikiana na kampuni hiyo katika kutekeleza mambo yote waliyokubaliana kwa lengo la kuhakikisha rasilimali ya madini inazinufaisha pande zote mbili.

Bristow alimhakikishia Rais Samia kuwa Barrick itaendelea kushirikiana na serikali kuimarisha uwekezaji kwenye sekta ya madini nchini na kuwa ipo tayari kuendelea kuwekeza katika maeneo mengine ya nchi.

”Tunaendelea vizuri na mkakati wa utekelezaji wa makubaliano baina yetu na serikali katika kuhakikisha pande zote mbili zinanufaika na rasilimali ya madini ya hapa nchini”alisema.

Bristow alisema Barrick imeajiri Watanzania wengi ikiwa ni pamoja na uongozi wa juu kama nafasi za Mkurugenzi Mtendaji, Meneja Mkazi na Mkuu Hesabu.

Pia alisema Barrick imeboresha usimamizi wa mazingira katika mgodi wa North Mara ikiwa ni pamoja na kuboresha mfumo wa kuhifadhia na kutibu maji yanayotokana na uzalishaji wa madini katika mgodi huo.

Alisema kwa sasa Barrick imeongeza ushiriki wa Watanzania katika kutoa huduma mbalimbali katika migodi yao ambapo takribani asilimia 70 ya manunuzi yanatoka hapa nchini.

Chanzo: www.habarileo.co.tz