Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mikasa, mateso yanayowakuta watoto wenye vichwa vikubwa na wazazi wao

Sfdv Mikasa, mateso yanayowakuta watoto wenye vichwa vikubwa na wazazi wao

Thu, 11 Nov 2021 Chanzo: Nipashe

FAMILIA nyingi nchini zenye watoto waliozaliwa na kichwa kikubwa (hydrocephalus) zinateseka kutokana na kunyanyapaliwa, pia kufiwa na watoto kwa kukosa fedha za kuwatibu, ingawa ni ulemavu unaozuilika.

Daktari bingwa wa upasuaji watoto, Petronilla Ngiloi, anasema chanzo kikubwa cha mtoto kuzaliwa na kichwa vikubwa ni mama kubeba ujauzito wakati mwili hauna madini ya folic acid.

Anasema kuzuia mtoto asizaliwe akiwa na kichwa kikubwa, mama anapaswa kabla ya kubeba ujauzito awe amekula vyakula vyenye virutubisho vya madini hayo, angalau miezi sita mfululizo na aendelee kula wakati wote wa ujauzito na baada ya kujifungua.

Daktari huyo anasema, wanawake wenye umri wa kubeba mimba na Watanzania wote wanaweza kuondokana na ukosefu wa madini hayo mwilini, kama serikali itachukua hatua kuweka madini hayo kwenye mlo unaotumiwa na wengi, mfano chumvi.

Anasema inawezekana, kwa sababu huko nyuma serikali ilishachukua hatua kama hiyo kuweka madini ya iodine kwenye chumvi kuzuia umma usipate ugonjwa wa tezi la shingo (Goita).

“Kwa sababu watoto wengi wanaozaliwa na kichwa kikubwa ni wale wa familia ambazo hazina uwezo,’’ anasisitiza bingwa huyo wa tiba magonjwa ya watoto wadogo.

Dk. Ngiloi anatoa mfano nchini Uholanzi walikofanikiwa kudhibiti watoto kuzaliwa na ulemavu huo, baada ya serikali kuamua kuweka madini ‘folic acid’ kwenye mlo wao unaotumiwa na wengi ‘cheese.’

Hadi sasa, Tanzania imo katika nchi za Afrika Kusini mwa Janga la Sahara zinazosumbuliwa na tatizo la watoto kuzaliwa na ulemavu wa kichwa kikubwa na taarifa za kimtandao zinabainisha ukanda huo unapata watoto aina hiyo 100,000 kila mwaka.

Daktari Ngiloi, anasema Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), hupokea watoto kati ya 300 na 400 kwa mwaka wenye tatizo hilo.

GHARAMA KUBWA

Dk. Ngiloi anasema mtoto anayezaliwa na ulemavu wa kichwa kikubwa, huhitaji matibabu ya upasuaji aweze kuwekewa mrija maalum unaojulikana kitaalamu kama “ventriculoperitoneal shunt (VPS)” wenye uwezo wa kuondoa maji kichwani kila wakati na kumuwezesha kuishi.

Anasema kabla ya kufanyiwa upasuaji, wanaanza na kipimo cha ‘X-ray’ kufahamu undani wa tatizo. Dk. Ngiloi anafafanua: “Matibabu haya ni ya gharama kubwa, yanaweza kufikia Sh. milioni moja na zaidi.”

JICHO KWENYE MKASA

Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na lishe bora kwa watoto wenye ulemavu (NPCD) Kanda ya Ziwa, Millicent Lema- Lasway, anasema wamebaini familia zenye watoto wenye ulemavu wa kichwa kikubwa na mgongo wazi (spinalbifida) zinashindwa kumudu gharama za matibabu, hata kusababisha vifo vya watoto wao.

Millicent anatoa ufafanuzi wa watoto wawili kutoka Kanda ya Ziwa, Ayub (mwaka mmoja) na Bhoke (11), ambao NPCD iliwasaidia baada ya familia kukwama fedha za matibabu na wamefariki dunia kwa saabu hawakupata tiba kwa wakati.

Baba mzazi wa Ayub. Japheti Bwegamo wa Kijiji cha Kisanghwe, Kata ya Butundwe mkoani Geita, anaiambia Nipashe kwa njia ya simu kwamba mwanawe alizaliwa Desemba 27 mwaka 2019, katika zahanati ya kijiji hicho alikogundulika na kidonda mgongoni.

Kwa mujibu wa Dk. Ngiloi, mtoto anapozaliwa na kidonda mgongoni(spinalbifida) ni dalili kwamba ana tatizo la kichwa kikubwa.

Bwegamo anafafanua kwamba baada ya kugundulika na hilo tatizo, aliwapatiwa rufani kwenda hospitali ya wilaya ambako nako akapewa rufani kwenda Hospitali ya Mkoa Mwanza,

”Baada ya kupokewa hospitalini, kesho yake mtoto alipimwa kichwa tukalipa elfu thelathini, vipimo na elfu thelathini za dawa ya kupaka kwenye kidonda, kasha,” anaeleza, pia akiwa na ufafanuzi wa malipo ya mtoto kukaa hospitalini hapo kwa siku tano.

Anasema baada kutumia dawa, kidonda kilipona isipokuwa walilazimika kurudi tena hospitali, maana kichwa cha mtoto kilianza kuvimba na kinachobonyea.

Baba huyo anasimulia mtoto wake (Ayubu) alifanyiwa upasuaji Januari 25, mwaka jana, kwa malipo ya Sh. 300,000 za vipimo, upasuaji na kumuwekea mrija kutoa maji kichwani.

Anasema mtoto alidumu wodini mwezi mmoja akilipia fedha zake. Anaendelea: “Sikumbuki ni Sh. ngapi, lakini walikuwa wanatuambia tunacholipa ni kidogo, maana kama mtoto angekuwa amezidi miaka mitano tungelipa fedha nyingi, ingeweza kufika hata milioni tatu au nne.”

Mzazi huyo anasema, baada ya mtoto kupata nafuu, miezi kadhaa tatizo lilirejea, maana mirija aliyowekewa kutoa maji kichwani iliziba hata kabla ya siku aliyopangiwa kurejea hospitalini kwa uangalizi, Agosti 31, mwaka jana.

Anasema akiwa na mkewe walipompeleka hospitalini walitakiwa kulipa Sh. 300,000 za kufanyiwa upasuaji wa pili, kuwekewa mrija mwingine.

“Hali yetu kifedha ilikuwa mbaya, maana tuliondoka nyumbani na laki moja, elfu arobanini tukawa tumetumia nauli watu wawili mimi na mke wangu na tulikuwa tumebakiwa na elfu sitini tu tukakataliwa tukaambiwa tulipe angalau Sh.150, 000,” anaeleza Bwegeno.

Anasema kutokana na kukosa fedha, mtoto hakupata matibabu na walirudi nyumbani kijijini, mtoto akiendelea kuwa na hali mbaya.

Bwegeno, anasimulia kwamba wakiwa nyumbani, walipokea simu kutoka hospitalini Bugando ambako NPCD waliwaaka wafike huko mgonjwa wahudhurie semina wakiwa na mtoto wao.

“Tuliwaambia hatuna uwezo wa kuja hatuna nauli. Waliniomba nitafute nauli angalau mama aende akiwa na mtoto, NPCD itamrejeshea,” anaeleza Bwegeno

Anafafanua mkewe alienda na alipofika huko, mtoto huyo alikuwa na hali mbaya na ndipo NPCD ikaamua ichangishe fedha za kumgharamia mtoto vipimo, upasuaji, kuwekewa mrija mpya na gharama za kukaa hospitali siku tano.

Hata hivyo, Bwegemo anasema walipata huduma na baada ya kufika nyumbani, kidonda cha upasuaji hakikuopona na hali ya mtoto iliendelea kuwa mbaya na kwa vile hali yao kifedha ilikuwa mbaya, walishindwa kumrudisha hospitalini na mtoto alifariki Novemba 9, mwaka jana, ikimaanisha leo inatimu mwaka mmoja na siku mbili.

MZAZI MWINGINE

Baba wa Bhoke, Zablon Maitari, anasimulia Nipashe kwa njia ya simu mkasa wake kutoka kijijini Nyamakobiti, kata ya Majimoto, wilayani Serengeti, mkoa Mara kwamba yeye na mkewe wameteseka sana kumhudumia mtoto wao.

“Tatizo la Bhoke lilikuwa kubwa. Alikuwa na kichwa kikubwa na mgongo wazi...mgongo ulikuwa na shimo, palitoa maji kila wakati.

“Kulikuwa hakuna mawasiliano kutoka kiunoni hadi miguuni kwa mtoto. Alihitaji matibabu na uangalizi wa karibu wakati wote,” anaeleza Matairi.

Anasema mtoto wake alifanyiwa upasuaji na kuwekewa mrija (shunt) akiwa na miaka mitatu lakini akiwa na umri wa miaka tisa iliziba akafanyiwa upasuaji kuwekewa mwingine.

“NPCD ndio walitutafutia pesa kulipia vipimo, kumfanyia mtoto upasuaji na gharama za kukaa hospitali siku mbili siku ya tatu tukaondoka kwenda nyumbani,” anasema Maitari.

Anafafanua mtoto wake aliporudi nyumbani, hali yake ilikuwa mbaya zaidi, maana mrija (shunt) aliyowekewa iligoma kufanya kazi na ndani ya wiki tatu walimrudisha hospitalini.

Mzazi huyo anasema, alikaa hospitalini wiki nzima akihudumiwa, akigusia la kipekee: “Alikuwa na maumivu makali sana, kila siku alilia ‘ninakufa’ ‘ninakufa’ na akafa tarehe thelathini, mwezi wa nne 2021.”

Mama wa Bhoke, Mkwami Matiko, anaendeleza simulizi akimsifu mumewe katika miaka yote 11 ya Bhoke, alijitoa kikamilifu kumlea mwanawe, kinyume na baadhi ya wanaume wanaonyanyapaa familia, penye mikasa ya ulemavu kama huo,

“Hata Bhoke alipokufa, mume wangu ndiye alikuwa naye hospitali, maana mimi nilikuwa mjamzito,’’ anasimulia.

ANGALIZO LA WADAU

Wadau asasi ya NPCD, inaeleza kuguswa na kifo cha Bhoke katika imani huenda uhai wake ungedumu, iwapo angepatiwa matibabu ya ziada na uangalizi wa karibu wa kitabibu hadi kupona majeraha na kuhakikisha mrija mpya aliyowekewa, umekubalika vyema mwilini.

“Ninaamini mikiki ya kusafiri siku ya tatu baada ya upasuaji tena umbali mrefu kwenye mabasi kutoka Mwanza hadi vijijini mkoani Mara inawezekana kulikuwa na athari mbaya kwa mtoto’’ anasema Millicent, Mkurugenzi wa NPCD.

Ikirejewa Sera ya Taifa ya Afya ya Mwaka 2017, inalenga kukabili magumu ya afya yanayowakabili wananchi maskini, hasa kuhusiana na kupata fedha za huduma ya afya.

Hapo ndipo penye angalizo la Dk. Ngiloi, akitaka kuwapo mfuko maalumu wa matibabu ya watoto wanaozaliwa na ulemavu kichwa kikubwa, ili wapatiwe tiba kamili hadi kuruhusia kuondoka hospitalini.

Bingwa huyo anasema, watoto wanaozaliwa na vichwa vikubwa wakipatiwa bima za bure na kukawepo na fungu maalum la fedha kuilipia, watakuwa na uhakika wa tiba; kupimwa, kufanyiwa upasuaji na kulazwa hospitalini.

Ni ushauri unaoungwa mkono na Mwenyekiti wa kijiji cha Kasanghwa, Tiro Wakayeye Wasigara, wanakopatikana wazazi wa marehemu mtoto Bhoke.

Wasigara anasema, watoto wenye ulemavu pia wanahitaji kusaidiwa pia huduma nyingine kama baiskeli wamudu maisha yao, akitoa mfano wa kuwapo mtoto kijijini anayeteseka na madhila hayo.

Chanzo: Nipashe