Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Michepuko, ngono zembe chanzo saratani ya kizazi

Saratani Agizo Michepuko, ngono zembe chanzo saratani ya kizazi

Sat, 19 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu ambao wana wapenzi wengi na wanafanya ngono bila kinga yoyote, wapo katika hatari kubwa kupata kirusi kiitwacho Human Papilloma Virus (HPV), ambacho kinahusishwa kuwa chanzo kikuu cha saratani ya mfumo wa uzazi wa mwanaume na mwanamke.

Hayo yamesemwa na daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Caroline Swai, wakati wa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari wiki hii, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa utoaji habari za afya hususani ugonjwa wa saratani.

Mafunzo hayo ni Mradi Mtambuka wa Saratani (TCCP), unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa na Aga Khan Foundation.

Dk. Caroline anasema wanaume ndio wasambazaji wakubwa wa virusi vya HPV kwa kutoa kwa mwanamke mmoja kwenda kwa mwanamke mwingine, wakati wa kujamiana.

“Ndio maana tunasema kuwa na mpenzi mmoja mwaminifu, mfano mwanaume ana wanawake wawili au watatu au zaidi, katika hao wanawake mmoja akitokea ana kirusi cha HPV, basi mwanaume atakapojamiiana nae bila kutumia kinga, atakibeba kirusi, akienda kukutana na mwanamke mwingine anakihamishia kwake, mwisho wa siku ile cheni ya wanawake zake wote ambao wanafanya naye ngono zembe wanapata ugonjwa,” anasema

Anasema kwa Tanzania, saratani ya shingo ya kizazi ndio inayoongoza kwa wanawake, kwani kwa mwaka 2020 takwimu zinaonesha kuwa maambukizi mapya yalikuwa 10, 241 ambayo ni sawa na asilimia 25.3 na vifo ni asilimia 24.2.

“Takribani wanawake 9,772 hugundulika kila mwaka kuwa na saratani ya mlango wa kizazi,” amesema.

Anasema kuwa mbali na ngono zembe, pia kuanza kufanya ngono katika umri mdogo chini ya miaka 18 nayo huchangia saratani ya shingo ya kizazi.

Pia kuwa na upungufu wa kinga ya mwili, matumizi ya pombe na tumbaku pamoja na maambukizi mengine yakiwemo magonjwa ya zinaa kama kisonono, kaswende na Ukimwi.

Dalili:

Kwa mujibu wa daktari huyo dalili za mtu mwenye saratani ya shingo ya kizazi ni kupata hedhi kwa mzunguko usio wa kawaida au kutoka damu baada ya kujamiana, maumivu ya mgongo, mguu na fupanyonga, uchovu, kupungua kwa uzito na kutokuwa na hamu ya kula, maumivu kwenye uke au kutoa harufu mbaya ikiwa ni pamoja na kuvimba kwa mguu mmoja

Uchunguzi:

Amesema uchunguzi wa virusi hivyo unastahili kufanyika, ili kuvigundua mapema na matibabu yake yanategemea na viwango vya virusi hivyo mwilini.

Hata hivyo anasema yanaweza hitaji kutibiwa kwa njia ya upasuaji na kutoa sehemu au mfuko wa uzazi mzima au kutumia mionzi.

Pia ameshauri wazazi kuwapeleka mabinti zao kuanzia miaka 12 hadi 14 kupatiwa chanjo ya HPV, ili kupunguza athari za ugonjwa huo kwa mabinti.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live