Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miaka mitano ya mfanikio Hospitali ya Benjamin Mkapa

0fc8468a67dc0dca156b12f34da57776 Miaka mitano ya mfanikio Hospitali ya Benjamin Mkapa

Tue, 24 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

HOSPITALI ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma imekuwa hospitali maarufu katika Kanda ya Kati kutokana na kusafisha na kupandikiza figo kwa wagonjwa waliobainika kuwa na tatizo la figo kushindwa kufanya kazi.

Akizungumza hivi karibuni katika kumbukumbu ya miaka mitano tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Alphonse Chandika alisema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na uvumilivu na moyo wa kujitolea.

Hospitali hiyo ndani ya kipindi cha miaka mitano tangu 2015, imekuwa tegemeo kubwa kwa wananchi mbalimbali kutokana na kupiga hatua kubwa kwa kupanua huduma zake, kuongeza watumishi na hasa ya kufaulu kupandikiza figo kwa wagonjwa.

Dk Chandika alisema katika kipindi hicho cha miaka mitano wamejikita katika kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi wa mkoa wa Dodoma, mikoa jirani na Tanzania kwa ujumla kwa magonjwa ambayo hapo awali wagonjwa walisafirishwa kwenda nje ya nchi.

"Baadhi ya huduma ambazo zinazotolewa katika hospitali hiyo ni za kibingwa bobezi zikiwemo za kusafisha damu kwa wagonjwa ambao figo zao zinakuwa zimeshindwa kufanya kazi," alisema.

Katika kuhakikisha wanafanikisha usafishaji wa damu, tayari hospitali hiyo imefunga mashine 11 na zinafanya kazi ya kusaidia jamii kupata huduma hiyo katika hospitali hiyo.

Dk Chandika alisema mwaka 2018, hospitali hiyo pia ilianza kupandikiza figo kwa msaada wa watalaamu kutoka Japan na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), baadaye watalaamu wa ndani wameendelea kupandikiza figo na hadi sasa imepandikiza figo wagonjwa 13 kati yao wawili wakipandikizwa na watalaamu wa ndani.

Dk Chandika alisema, hospitali hiyo pamoja na kufikia hatua ya kuwa hospitali bora kanda ya kati, ilianza na watumishi wa kuazima kutoka katika hospitali jirani ikiwemo ya General Dodoma na Kituo cha Afya cha Makole.

Pia ilianza na watumishi 22 ambao kati yao wengine walikuwa wa kuazima na kutokana na jitihada za serikali sasa ina watumishi 453.

Mmoja wa wauguzi waanzilishi wa hospitali hiyo, Debora Mabwasa alisema anajisikia fahari kuwa sehemu ya mafanikio ya hospitali hiyo ndani ya kipindi cha miaka mitano tangu kuanzisha kwake.

Alisema hali imebadilika sana kwani hapo awali kutokana na uhaba wa vifaa katika hospitali hiyo walilazimika kuazima vifaa vingine kutoka katika hospitali nyingine ili wawatandikie wagonjwa.

Alisema awali kutokana na uchache wa watumishi, hakukuwa na zamu hivyo watumishi iliwalazimu kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba wanatoa huduma kwa wagonjwa waliokuwa wanafika hospitalini hapo.

Mtumishi mwingine aliyekuwepo wakati inaanza, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji katika Hospitali hiyo, Dk Januarius Hinju alisema ilibidi wahamishe baadhi ya wagonjwa kutoka hospitali ya General ili kuruhusu Rais Jakaya Kikwete (wakati huo) aifungue baada ya kueleza hatofungua majengo bali hospitali inayotoa huduma kwa watu.

Hospitali ya Benjamini Mkapa iliasisiwa na Rais mstaafu Kikwete na ikazinduliwa naye mwaka 2015 ikiwa na lengo la kupunguza gharama kwa Serikali za kupeleka wagonjwa nje ya nchi.

Tangu wakati huo inatumika kama Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kati baada ya kufungwa vifaa tiba vya kisasa ambavyo vingine havipatikani katika hospitali nyingine.

Chanzo: habarileo.co.tz