Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mhudumu wa Afya abuni kitanda cha kupakia na kushusha mgonjwa kwenye gari

Mhudumu Kitanda Mhudumu wa Afya abuni kitanda cha kupakia na kushusha mgonjwa kwenye gari

Tue, 12 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amezindua kitanda kinachojongea ambacho kinatumika wakati wa kumshusha na kumpakia mgonjwa kwenye gari la wagonjwa ambacho kimetengenezwa na Mhudumu wa Afya Bw. Erasto Francisco kwa lengo la kusaidia kutatua changamoto wanazokutana nazo wanapotoa huduma hiyo.

Akizungumza wakati wa kupokea kitanda hicho Prof. Janabi amesema kazi ya kumpakia na kumshusha mgonjwa kwenye gari ni kazi yenye changamoto nyingi kwakuwa wagonjwa wengine wanakuwa na uzito mkubwa na endapo mtumishi atafanya kazi hiyo kwa muda mrefu inaweza kumsababishia kupata matatizo ya mgongo.

“Nampongeza sana Bw. Francisco kwani amekuja na ubunifu mkubwa ambao unaendea kutatua changamoto kwa watoa huduma za afya hapa Muhimbili vilevile ubunifu huu utaenda kunufaisha watoa huduma wa afya katika hospitali zingine nchini” amesema Prof. Janabi.

Awali akizungumza kabla ya kukabidhi kitanda hicho Bw. Francisco amesema kuwa alipata wazo la kutengeneza kitanda hicho baada ya kuona changamoto wanazokutana nazo watoa huduma wakati wa kumshusha mgonjwa kutoka kwenye gari na kumpelekea wodini.

“Changamoto iliyonifanya nibuni kitanda hiki ni pale mgonjwa anaposhushwa anaweza kupata maumivu makali wakati wa kumshusha kutoka kwenye gari la wagonjwa na kumuweka kwenye kitanda cha nje pia wakati mwingine mgonjwa anaweza kudondoka,” amesema Bw. Francisco .

Prof. Janabi amewasisitiza watumishi wa Muhimbili kuendelea kuwa wabunifu na kuja na mawazo ambayo yatasaidia kutatua changamoto mbalimbali ili kuenedelea kuboresha huduma za afya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live