Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Mgonjwa ana haki ya kuishtaki hospitali, mtaalamu siri zake zikivuja’

HUKUMU ‘Mgonjwa ana haki ya kuishtaki hospitali, mtaalamu siri zake zikivuja’

Tue, 24 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali kupitia Ofisi ya Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imesema mteja ‘mgonjwa’ ana haki ya kukishtaki kituo cha afya, mtumishi wa maabara au daktari iwapo vipimo vyake vya maabara vitavuja kwa mtu mwingine bila ridhaa yake.

Hayo yanaelezwa kukiwa na malalamiko ya chinichini ya kutokuwepo kwa usiri miongoni mwa kundi la vijana ambao hufika vituo vya afya kwa ajili ya kuhitaji huduma za afya ya uzazi ikiwemo kupima magonjwa ya zinaa na Ukimwi.

Tamisemi imeyasema hayo leo Jumanne, Oktoba 24, 2023 na Ofisa Mteknolojia maabara kutoka Ofisi ya Rais – Tamisemi, Peter Torokaa alipokuwa akitoa mara kuhusu huduma za maabara.

New Content Item (1) New Content Item (1)

Amesema wataalamu wa maabara wamepewa umiliki wa nyaraka za wateja, taratibu zote za kuchakata sampuli kuanzia kupokea mpaka kupata majibu kwa kufuata taratibu na siri ni miiko ya kitaaluma.

“Mgonjwa ana wajibu na haki za kushtaki kwa kutoa siri zake, mtaalamu anatakiwa kukaa na mgonjwa pekee ndipo ampe majibu yake haijalishi ana kipato au hali yake ya kiuchumi lakini akishafikisha umri wa miaka 18 anatakiwa kupewa majibu yake yeye ataamua amshirikishe nani,” amesema Torokaa.

Amesema iwapo mgonjwa atatoa ushahidi wa siri za ugonjwa wake kuvuja kwa watu wengine baada ya vipimo, sheria itafuata mkondo wake ambapo atatakiwa kulipwa faini au kifungo kwa mtuhumiwa au vyote kwa pamoja.

Hata hivyo Torokaa amesema kuna uwezekano kwa wataalamu wao kwa wao kushirikishana majibu ya mgonjwa ikiwa kuna changamoto hasa katika magonjwa ambukizi ili kulinda usalama wa wataalamu wengine.

“Ili kujikinga sisi wataalamu husika tutashirikishana kwa maana sampuli inashikwa na wataalamu wengi na hufanya hivyo kuepuka athari kwa wataalamu kwa ajili ya usalama lakini isihusishe watu wengine.”

Amesema mtaalamu akigundulika kufanya kosa hilo atapelekwa mahakamani na kwamba majibu si ya maabara pekee bali ni majibu ya mgonjwa anauwezo wa kuyaomba akapewa lakini hatakiwi kuyatangaza.

“Majibu ukipewa hutakiwi pia kuyarusha mtandaoni au popote kwa kufanya hivyo pia ni kinyume cha sheria hospitali au maabara husika nayo pia inalindwa kisheria itakushtaki.”

Torokaa amesema watumishi wa maabara wanazalishwa vyuo vilivyosajiliwa kupitia baraza la Wataalamu wa maabara kwa mujibu wa sheria namba 22 ya mwaka 2007, hivyo mafunzo ya kutunza siri za wagonjwa ni miongoni mwa yale waliyofunzwa.

Amesema pia huendelea kupata mafunzo makazini na kupimwa umahiri, pia husaini viapo vya utunzaji siri na miiko ya taaluma.

Daktari wa Hospitali ya taifa Muhimbili, Koga Luhulla amesema mgonjwa anapoenda kwa daktari majibu ni haki yake, kama anataka kuondoka na majibu yake atapewa ingawa wagonjwa wengi bado hawajui haki zao.

“Unapoenda hospitali za ngazi ya chini ukaona unapimwa kila siku bado unaendelea kuumwa una haki ya kuomba vipimo vya juu na ukapelekwa hospitali ngazi za juu kupimwa maabara upya au kupata vipimo vya ziada na pia kuulizia majibu ujue tatizo ni nini kwani Tanzania madaktari ni wachache kama mgonjwa asiposema anahitaji nini ni changamoto,” amesema Dk Koga.

Mkuu wa uchunguzi wa huduma za afya, Tamisemi Fedinand Matata akielezea huduma za uchunguzi za maabara katika afya ya msingi amesema iwapo siri za mgonjwa zitatoka, kuna mashauri mawili yanaweza kufanyika.

“Mtaalamu utapelekwa mahakamani. Pia kuna mabaraza ya kitaaluma ambayo yanashughulikia utendaji kazi wa wataalamu katika taaluma husika mojawapo ni kufutiwa leseni ya taaluma husika na mwajiri atafuata sheria kulingana na utumishi wa umma.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live