Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgonjwa aliyepona corona anaweza kupata mara ya pili? Jibu hili hapa

100861 Pic+corona+kupona Mgonjwa aliyepona corona anaweza kupata mara ya pili? Jibu hili hapa

Tue, 31 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ofisa programu wa elimu ya afya kwa umma nchini Tanzania, Dk Tumaini Haonga amesema bado hakuna ushahidi wa kisayansi unaobainisha kuwa mgonjwa aliyepona maambukizi ya korona hawezi kuambukizwa mara ya pili.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Machi 31, 2020 Dk Haonga amesema kuwa bado wataalam wanafanya uchunguzi kubaini uhusiano uliopo kati ya mgonjwa alieyepona maambukizi ya corona na kama anaweza kupata maambukizi hayo mara ya pili.

Ugonjwa wa corona ni ugonjwa wa mlipuko unaosababishwa na virusi vya covid-19 ambao umeanzia nchini China mwishoni mwa mwaka jana.

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu leo Jumanne ametangaza kifo cha kwanza cha mgonjwa wa corona kilichotokea katika kituo cha matibabu cha Mloganzila jijini Dar es salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya waziri huyo mpaka sasa Tanzania imebaini wagonjwa 19 wa corona ambapo mgonjwa wa kwanza kugundulika na maambukizi hayo tayari ameshapona.

Katika mazungumzo na Dk Haonga ambayo Mwananchi ilimtafuta kupata ufafanuzi wa mambo kadhaa yanayohusiana na wagonjwa wanaopona maradhi hayo ikiwa ni pamoja na kama maambukizi yanaweza kumrudia mgonjwa aliyepona? Dk Haonga amesema kuwa bado uchunguzi unafanyika kubaini kama mgonjwa aliyepona corona anaweza kupata maambukizi kwa mara ya pili.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Huu ugonjwa wa corona bado ushahidi wa kisayansi haujajengwa wa kusema kuwa mtu akipata hayo maambukizi hawezi kupata tena, kama mnavyofahamu huu ugonjwa bado ni mpya kwa hiyo vitu vingi bado vinafanyiwa kazi," amesema mtaalamu huyo.

Amesema kuwa uzoefu uliopo mwili unajijengea kinga wenyewe baada ya kupata ugonjwa hasa katika magonjwa yanayosababishwa na virusi.

“Magonjwa mengi hususani yanayosababishwa na virusi mwili huwa unajenga kinga wenyewe ya aina ileile ya kirusi ambacho mtu atakuwa aliumwa kwa hiyo kirusi kama hichohicho kikaja baadaye mwili unakuwa tayari umejiimarisha kupambana na hicho kirusi na hatimaye mtu hawezi kuumwa,” amedokeza

“Ili kufikia hali ya kutambua kuwa mtu akiumwa mara ya kwanza hawezi kuumwa tena ni mpaka kuwafuatilia watu wengi waliopata ugonjwa wakapona lakini wakawa kwenye mazingira ambayo wanaweza kuambukizwa ili kuweza kuona miili yao imejenga kinga au haijajenga.”

Amesema wapo wataalamu ambao wanafanya uchunguzi kwa waliopona ugonjwa huo ili kubaini kisayansi.

“Kuna watu ambao ndio wanafuatilia saa hivi kwa waliopata maambukizi mwanzoni na wakapona na kuona kuwa wanaweza wakapata tena”

“Lakini Japan kulikuwa na mgonjwa ambaye alikuwa ameumwa badaye akapona, lakini baadaye akaja kuonekana kuwa ana virusi, sasa baada ya kuchunguza ilionekana kuwa yule mgonjwa virusi vilikuwa havijatoka kabisa mwilini"

“Kwa hiyo kwa yule ambaye alikuwa amepona kabisa kuwa anaweza kupata tena hilo bado hatujapata ushahidi wa kutosha wa kisayansi.”

Amesema magonjwa mengi yanayosababishwa na virusi mtu akishapata mara moja aina hiyohiyo ya kirusi hawezi kupata tena, akitolea mfano ugonjwa wa tetekuwanga au homa ya dengue ambayo ni miongoni mwa magonjwa mtu akishaumwa mara moja hauwezi kuumwa tena mara ya pili.

Kutokana na taarifa kuwa mpaka sasa ugonjwa huo hauna tiba wala chanjo, Mwananchi ilimuuliza Dk Haonga kuwa wagonjwa wanaopona wanatumia dawa gani?

Akijibu swali hilo, Dk Haonga amesema kuwa wagonjwa wanaotengwa karantini hawapewi dawa za moja kwa moja za kutibu corona kutokana na ugonjwa huo kutokuwa na tiba badala yake wanapewa dawa zinazotibu dalili au madhara ya yaliosababishwa na ugonjwa huo.

“Wagonjwa wanapowekwa karantini kule wanapewa tiba za kutibu dalili au madhara yanayoletwa na hiki kirusi mwilini, kwa kutibu dalili na madhara tayari unaupa mwili nguvu ya kuweza kupambana na hatimaye mwili unafanikiwa kuviondoa kabisa virusi hivyo, vinakufa na vinamezwa kabisa na seli za mwili,"amesema

“Kama mgonjwa anatapika atapewa dawa za kuzuia kutapika, kama anaumwa kichwa atapewa dawa za kutuliza maumivu lakini kama ameshindwa kupumua atawekewa mashine za kumsaidia kupumua, hicho ndicho kinachofanyika” amesema

Pia, amebainisha kuwa kitu kingine wanachopewa wagonjwa ni lishe bora ili kinga za mwili ziweze kupambana na kirusi hicho

“Wanapewa chakula ambacho ni mlo kamili ambacho ni eneo muhimu sana katika kufanya kinga ya mwili isishuke, huu ugonjwa kitakachompa mtu nafuu ni kinga ya mwili, mwenye kinga imara ana uwezo mkubwa wa kupambana na kupona,"amebainisha

Mtaalam huyo amesema kuwa kitu kingine wanachopewa wagonjwa waliotengwa karantini ni ushauri wa kisaikolojia ili mwili usidhoofike “Vilevile wanapewa unasihi wa kisaikolojia na akili inakuwa saawa na mwili haudhoofu."

Dk Haonga ametoa rai kwa jamii isitumie dawa yoyote wanapojihisi wanaumwa kabla ya kupata vipimo na ushauri kutoka kwa wataalum

“Sio kwamba kuna dawa maalumu wanazopewa wagonjwa wa corona, mtu gani apewe nini inatokana na dalili alizonazo mgonjwa, hivyo hatuwezi kusema wanavyopewa wagonjwa karantini vinaweza kufanyika kweneye jamii bila watalam wa tiba.”

Amesema kwa sasa muitikio kwa jamii wa namna ya kujikinga na maambukizi hayo ni mkubwa japokuwa ni maisha mapya katika jamii

“Muitikio ni mkubwa sana, hata ukitembea kwenye mitaa unaona watu wameweka sehemu za kunawia mikono, tunahitaji kuweka nguvu zaidi kwa sababu huu ni mfumo ambao ni mpya watu hawakuuzoea”

“Kikubwa tunachofanya ni kuwasisitiza wananchi kufuata masharti ili kwa kuwa ugonjwa upo nchini usije ukasambaa zaidi” amesisitiza Dk Haonga.

Chanzo: mwananchi.co.tz