Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgagani unavyotumika kusafisha damu na kuondoa sumu mwilini

Mgagani Ges (16).jpeg Mgagani unavyotumika kusafisha damu na kuondoa sumu mwilini

Fri, 5 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwili wa binadamu hauwezi kutengeneza vitamini A pekee, badala yake hutengeneza vitamini hiyo kupitia vyakula anavyokula.

Vyakula vinavyotengeneza vitamini A ni mboga za majani zenye rangi ya kijani pamoja na matunda.

Miongoni mwa vyakula hivyo vyenye rangi ya kijani ni mboga za majani za aina zote, ikiwemo mgagani.

Mgagani ni mboga ambayo mwanzo ilikuwa hailimwi, ilikuwa inapatikana porini tu, lakini siku hizi ni mboga ambayo wataalamu wa lishe wanaeleza ina faida nyingi.

Mtaalamu wa mimea asili na virutubisho tiba kutoka taasisi ya Fadhaget Nutrition Science, Dk Fadhili Emily anasema mboga za majani, ukiwemo mgagani na mchunga zina kitu cha kipekee kwa mwili wa binadamu kutokana na uchungu ulionazo.

Anasema mgagani ni mboga nzuri, japo baadhi ya familia hawaipi kipaumbele, lakini ikitumiwa kama chakula ina faida nyingi.

Dk Emily anasema mbali na chakula, mgagani ukitumika nje ya mfumo wa chakula, husaidia  kutibu magonjwa mbalimbali, ikiwemo vidonda kwa sababu ina kiwango kikubwa cha madini ya chuma, vitamini A na virutubisho muhimu.

“Uchungu uliopo katika mboga hizo una faida kiafya, miongoni mwa faida za mgagani katika mwili wa binadamu ni kusafisha damu na kuondoa sumu kuvu mwilini,” anasema.

Pia anasema wale ambao mwili umechakaa na unatengeneza fangasi, ulaji wa mboga hiyo husaidia kuimarisha kinga inayosaidia fangasi kuondoka.

“Kwa wanawake wanaowashwa katika via vya uzazi au kutoka uchafu katika via vya uzazi  na wale wenye fangasi katika vidole vya miguu, tumekuwa tukiwashauri watumie mmea huo ili kukabiliana ana changamoto hizo,” anabainisha.

Anasisitiza ulaji wa mgagani mara kwa mara husaidia mwili kuepuka changamoto za kiafya kwa sababu ni moja ya mboga muhimu ambazo zikitumika vizuri huzuia changamoto hizo.

Najma Mohamed, mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam anasema licha ya uchungu wa mboga hiyo, amekuwa akiitumia mara kwa mara baada ya kuelezwa faida zake kiafya.

“Ule uchungu wala siujali, pia mboga ya mgagani ukipika na ukiiweka na karanga za kusagwa au siagi, huwezi kuacha kutumia. Ni mzuri sana,” anasema Najma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live