Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfumo usalama watakiwa kwa wamiliki wa viwanda

Hadija Mfumo usalama watakiwa kwa wamiliki wa viwanda

Mon, 1 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAMILIKI wa viwanda nchini wametakiwa kuweka mfumo madhubuti wa kulinda afya na usalama wa wafanyakazi, kwa kuwa bado kuna changamoto nyingi za kiusalama katika maeneo yao ya kazi.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda, aliyasema hao wakati viongozi wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), walipotembelea ofisi za Osha kwa lengo la kujadiliana namna bora zaidi ya kuboresha mifumo ya usalama na afya katika viwanda hapa nchini.

“Kwa hiyo nilipenda nanyi mfahamu kwamba usalama katika viwanda vyetu haupo katika viwango stahiki kwa asilimia zote na ndiyo maana taasisi yetu imekuja na mpango mahususi wa kuzuia ajali katika sehemu za kazi ujulikanao kama ‘Vision Zero’ ambao endapo utatekelezwa ipasavyo katika viwanda na sehemu nyingine za kazi basi matukio ya ajali yatabaki kuwa historia,” alisema Mwenda.

Ujumbe huo wa viongozi kutoka CTI ambao ulijumuisha baadhi ya wawakilishi wa wanachama, uliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirikisho hilo, Leodgar Tenga.

Akizungumza baada ya kuhitimisha kikao hicho, Tenga alisema madhumuni ya kikao yalikuwa ni kujadiliana juu ya utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

“Tunafahamu kwamba OSHA ipo kwa mujibu wa sheria na ina kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba kunakuwa na usalama wa wafanyakazi katika maeneo ya kazi na wenye viwanda ndiyo wahusika wakubwa sana katika hili na kwa sababu hiyo tumekuja ili kuona ni kwa jinsi gani tutahakikisha wenye viwanda wanatimiza matakwa ya OSHA,” alisema Tenga na kuongeza:

“Kikao kilikuwa kizuri, tumebadilishana mawazo kwa uwazi kabisa, tumewaambia wenzetu wanachama wetu wanasema nini kuhusu utendaji wao na wao pia wamesema jinsi ambavyo wenye viwanda wanatekeleza sheria na pale ambapo pana upungufu kila upande, tumeuzungumza na hatimaye tumekubaliana kwamba ipo haja ya wenye viwanda kuelimishwa zaidi kuhusu hii sheria.”

Alisema kupitia kikao hicho wanatarajia kutakuwa na uelewa zaidi kwa pande zote mbili na kwamba; kwa upande wa OSHA wataelewa changamoto ambazo viwanda vinakumbana nazo na wenye viwanda wataelewa ni wanapaswa kufanya katika kuteleza sheria.

Veronica Mbazingwa, kutoka kampuni ya Chemicotex, alisema kikao hicho kimekuwa ni fursa nzuri kwao ya kujifunza jinsi ambavyo OSHA inashiriki kikamilifu katika kuwasaidia wawekezaji hasa katika kuhakikisha kwamba usalama wa wafanyakazi ambao ndiyo nguvu kazi kubwa katika uzalishaji wa viwandani unakuwa katika mtiririko unaotakiwa kisheria.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live