Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Meya: Vita ya unywaji pombe ianzie kwenye familia

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe ametaka mapambano dhidi ya unywaji wa pombe kupita kiasi kuanzia ngazi ya familia.

Amesema bora ianzie kwenye familia kwa sababu hata kama Serikali itatunga sera nzuri kiasi gani lakini kama jamii haitakubali kubadilika hakutakuwa na matokeo mazuri.

Profesa Mwamfupe ametoa kauli hiyo leo Oktoba 3, 2018 jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya kupinga unywaji pombe duniani yaliyofanyika kitaifa jijini hapa.

Amesema unywaji wa pombe kupita kiasi ni tabia ya mtu na hivyo inatakiwa kukomeshwa kuanzia ngazi ya chini ya familia hadi Taifa.

“Hakuna mtu asiyejua madhara ya unywaji pombe kupindukia, ikiwemo ajali za barabarani ambazo zinagharimu maisha ya watu ambao hata hawatumii pombe,” amesema Profesa Mwamfupe.

Aidha amesema kuwa unywaji huo wa  pombe unadhalilisha na kushusha hadhi ya mhusika mbele ya jamii.

Amesema watu wanywe pombe kistaarabu kama ilivyo kwa mila na desturi ambapo pombe zilikuwa zinakutanisha watu na kufurahi pamoja lakini si unywaji wa kupindukia.

Mbali na hilo amewataka wanawake wanaojishughulisha na utengenezaji wa pombe za kienyeji kutafuta shughuli nyingine za mbadala za kufanya badala ya kuendelea kutumia chakula cha familia kupikia pombe.

“Hawa wanawake wakipata shughuli nyingine mbadala za kufanya nje ya kutengeneza pombe za kienyeji tutaliepusha Taifa na ulevi wa kupindukia hasa vijijini ambako kuna nguvu kazi kubwa ya Taifa,” amesema Profesa Mwamfupe.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtandao wa kupambana na matumizi mabaya ya pombe (Taanet), Sofia Komba ameiomba Serikali kutunga sera itakayokataza matumizi ya pombe kupindukia kutokana na madhara  yanayotokana na unywaji huo.

“Kuna madhara makubwa yakiwemo magonjwa yasiyoambukiza na ya kuambukiza, ukatili wa kijinsia na hata kwa wanawake wanaweza kupoteza mimba zao kutokana na watoto kufia tumboni kutokana na unywaji pombe kupindukia,” amesema Komba.

Maadhimisho ya kupinga unywaji pombe duniani yalianza kuadhimishwa rasmi mwaka 2008 na leo ndiyo mara ya kwanza maadhimisho hayo kufanyika kitaifa nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz