Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge asimulia ‘alivyosulubiwa’ kwa kukataa kukeketwa

31596 Pic+mbunge Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Catherine Ruge

Fri, 14 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti. Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Catherine Ruge ameeleza matatizo aliyopitia baada ya kukataa kukeketwa

Amesema alilaaniwa na wazazi na wazee wa mila na kuelezwa na mganga wa kienyeji kuwa hangezaa kutokana na kukataa mila hiyo.

Akizungumza mbele ya wazee wa mila wa koo sita za Serengeti waliokutana kulaani na kuteketeza zana za ukeketaji eneo la Issenye, Catherine alisema ameamua kufanya hivyo kwa lengo la kumkomboa mtoto wa kike.

“Nilitakiwa kukeketwa na kuolewa nikiwa darasa la nne na baada ya kukataa, nililaaniwa na kuambiwa sitafaulu mitihani, kuolewa wala kuzaa,” alisema Catherine.

“Lakini nilisimama na Mungu na hatimaye nimefikia hapa nilipo.”

Aliwataka watoto wa kike kuepuka porojo za wazee wa mila na vitisho ambavyo alisema huishia kuolewa na kupoteza ndoto zao za maisha.

“Baada ya kufaulu masomo hadi chuo kikuu, niliolewa, lakini nilikaa muda mrefu bila kuzaa hivyo wengine wakaamini ni laana,” alisema.

“Ila mimi niliamini Mungu yupo na atanisaidia, muda tu ulikuwa haujafika. Sasa ni mama wa watoto wawili.”

Aliitaka Serikali kushirikiana kwa karibu na mashirika kama Amref Health Tanzania, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambao wanaendesha mradi wa Tokomeza Ukeketaji kwa ufadhili wa UN Women, ili kukabiliana na wanaokiuka Sheria.

Naye meneja wa mradi huo, Godfrey Matumu alisema kwa kipindi cha miaka mitatu kumekuwa na mafanikio, kama kupunguza idadi ya wanaokeketwa kwa asilimia 62, ikiwa ni tofauti na mwaka 2012.

Awali, katibu wa mila wa ukoo wa Watatoga, Girahuda Gesaga alisema wanatumia mfumo mpya ambao unaendeleza mila ya kuvusha rika, lakini bila ya ukeketaji ili kulinda mtoto wa kike.



Chanzo: mwananchi.co.tz