Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge amchongea daktari anayedaiwa kuomba rushwa wagonjwa

9959 Daktari+pic TZW

Mon, 25 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Handeni. Kaimu Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Msata, Mussa Muro amesema atayafanyia kazi malalamiko yaliyotolewa na mbunge wa Handeni (CCM), Mboni Mhita dhidi ya daktari wa kituo hicho pamoja na baadhi ya wauguzi.

Ametoa kauli hiyo jana Jumapili Juni 24, 2018 baada ya Mboni kufanya ziara katika kituo hicho cha afya na kueleza malalamiko kutoka kwa wananchi wanaodai daktari wa kituo hicho anawaomba rushwa wagonjwa, huku wauguzi wakiwanyanyasa wagonjwa kwa kuwaamrisha kupiga deki.

“Nimeyapokea maagizo yako nitayafanyia kazi kwa kushirikisha uongozi wa juu,” amesema Muro.

Katika maelezo yake Mboni amesema daktari huyo amechukua rushwa kwa mgonjwa ili aweze kumtibu, “niziombe mamlaka husika zimchukulie hatua huyu daktari ambaye anaomba fedha kwa wagonjwa ili amuhudumie, nasikia amehamishiwa hospitali ya wilaya ya Handeni. Asimamishwe huyu na uchunguzi ufanyike.”

Amesema kuhamishwa kwa daktari huyo si mwisho wa tatizo hilo na kusisitiza kuwa majukumu ya mtumishi si kuwakwaza na kuwanyanyasa wananchi.

“Mtumishi anapokosea katika kituo chake cha kazi uongozi wa idara husika unamuhamisha. Utaratibu huu si mzuri kwa sababu mhusika ametenda kosa na lazima achukuliwe hatua,” amesema Mboni

Amesema watumishi wa Serikali wanatakiwa kuwa makini kwa kuwa hivi sasa wananchi wanajua haki zao, kusisitiza kuwa taarifa za daktari huyo alizipata akiwa nchini Marekani, kwamba aliyemtumia ni mwananchi.

Mwajuma Athumani mkazi wa Mkata Handeni ametoa malalamiko mbele ya mbunge huyo, kubainisha kuwa wakati akiwa mjamzito, aliamrishwa na mtoa huduma wa maabara kupiga deki ili apatiwe matibabu na kwamba alitekeleza agizo hilo kwa kuwa alikuwa akihitaji kuhudumiwa.

 

 

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz