Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge ahoji wajawazito wanaotozwa fedha wakati wa kujifungua

3afef108440104cda09f9add261aa6f8 Mbunge ahoji wajawazito wanaotozwa fedha wakati wa kujifungua

Fri, 5 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKATI Serikali ikisisitiza matibabu bure kwa makundi ya wanawake wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na wazee kulingana na Sera ya Afya inavyosema, Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Emmanuel Mwakasaka amesema Hospitali ya Kitete mkoani Tabora wamekuwa wakiwatoza wajawazito Sh 30,000 hadi 50,000 wakati wa kujifungua.

Akiuliza swali bungeni leo Ijumaa Februari 5, 2020, Mwakasaka alihoji “Hospitali ya Kitete Tabora bado inatoza fedha kwa akina mama waliojifungua kwa njia ya kawaida na wanaoshindwa kutoa hizo fedha huwa wanazuiliwa. Je serikali ina msimamo gani kwa akina mama wanaozuiliwa kutoka na watoto wao wachanga hadi walipe?"-

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk Godwin Mollel amesema msimamo wa Serikali imeweka katika sera kuwa matibabu ya wanawake hao wanaojifungua bure na kuwataka waganga wa mikoa kuhakikisha wanasimamia suala hilo.

Amesema hospitali hiyo hukusanya Sh milioni 73 kama gharama za matibabu, Sh milioni 133 za Bima ya Afya na Sh milioni 34 kutoka Serikalini na hivyo kuwa na Sh milioni 260 kwa mwezi.

Amesema Sh milioni 13 ni matumizi yanayotokana na huduma zinazotolewa bure ikiwemo wanawake wanaojifungua na Sh milioni 134 kwa ajili ya matumizi mengine na hivyo kubakiwa na Sh milioni 120.

Amesema hakuna sababu ya kumtoza mama fedha wakati wa kujifungua kwasababu wameshalipiwa gharama hizo.

Hatahivyo, ameahidi kuongozana na mbunge huyo kwenda kupiga hesabu kwa pamoja na hatimaye watakubaliana na kuja na nini kifanyike baadaye.

Kwa mujibu wa Sera ya Afya wazee wenye umri wa kuanzia miaka 60, wajawazito na watoto chini ya miaka mitano wanatakiwa kupata huduma ya afya bure wanapokwenda hospitalini.

Sera hiyo ya mwaka 1990 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2009, inayatambua makundi hayo kwenye jamii kwamba yanatakiwa kupata matibabu bure kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali za serikali.

Chanzo: habarileo.co.tz