Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge Mattembe agawa vitanda, mashuka

21290 MATEMBE+PIC TanzaniaWeb

Mon, 8 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Singida. Kasi ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe kuboresha huduma za afya na miundombinu ya elimu, imetakiwa kuigwa na wanasiasa wengine waliopewa wadhifa kwa ajili ya kuwatumikia watanzania.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Singida, Eliah Digha wakati wa hafla ya mbunge huyo kukabidhi msaada wa vitanda (double decker) 20 kwa ajili ya hosteli ya wanafunzi wa kike kwenye Sekondari ya Mwanamwema Shein.

Mbali na vitanda hivyo, pia Mattembe alikabidhi msaada wa mashuka 50 na vifaa tiba kwenye Kituo cha Afya Mgori kilichopo Singida Vijijini ikiwa ni mwendelezo wa mkakati wake katika kuunga mkono jitihada za Serikali kuboresha huduma za afya mkoani Singida.

Digha ambaye alikuwa miongoni mwa waalikwa kwenye hafla hiyo, alisema katika kipindi cha miaka miwili tu tangu amechaguliwa kuwawakilisha wanawake wa Singida bungeni, Mattembe amefanya kazi kubwa ambayo haijapata kufanywa na watangulizi wake.

"Huu ndio uwakilishi ambao wananchi na wanawake wa Singida walikuwa wameukosa kwa miaka mingi iliyopita, lakini kupitia kwako (Mattembe) sasa hivi wanawake wanapata huduma bora. Si tu kuzungumza kila wakati kero za maji, huduma bora za afya na uwezeshaji vijana na wanawake, lakini binafsi umekuwa ukijitoa kwa hali na mali kwa kutumia kidogo ulichonacho kuwaletea watu wetu maendeleo. Hawa ndio viongozi wa kupigiwa mfano, " amesema Digha.

Kwa upande wake Mattembe amesema kuwa aliwahi kufanya ziara katika shule hiyo yenye kidato cha tano na sita kwa ajili ya wasichana pekee na kushuhudia changamoto za uhaba wa vitanda ambako aliahidi kuipatia ufumbuzi changamoto hiyo ili kuwawezesha watoto kusoma kwa utulivu.

"Kama rais wangu John Pombe Magufuli alivyojitoa kwa ajili ya kuliletea taifa maendeleo ya haraka nami lazima niunge mkono jitihada hizo ni ndio sababu niko hapa leo kuwasilisha msaada huu, kazi inaendelea kufanyika hadi kieleweke hapa," amesema Mattembe.

Kabla ya kukabidhi msaada huo, Mattembe pia alitembelea Sekondari ya Kinambeu iliyopo Iramba, ambayo jengo la hosteli ya wanafunzi wa kike liliteketea kwa moto kutokana na hitilafu ya umeme na kuharibu mali za wanafunzi.

Katika ziara yake hiyo alizungumza na wanafunzi, walimu na wazazi ambapo alikabidhi msaada mbalimbali ikiwemo ndoo, sabuni, mashuka na taulo za kike.

Chanzo: mwananchi.co.tz