Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Afya nchini Tanzania, Dk Faustine Ndungulile amesema kuna mabadiliko ya tabia za mbu kung’ata binadamu, wakiwemo wanaoeneza ugonjwa wa dengue.
Amesema waliokuwa wanang’ata usiku au jioni kwa sasa wanang’ata mchana na asubuhi, waliokuwa wanapiga kelele zaidi wakipita sikioni kwa sasa hawafanyi hivyo na wale waliokuwa wakiruka juu kuzidi usawa wa gari dogo kwa sasa wanaruka chini zaidi.
Ametoa kauli hiyo jana Jumanne Julai 9, 2019 baada ya kutembelea taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara hiyo katika maonyesho ya kimataifa ya biashara yanayofanyika katika viwanja vya Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
“Kuna mbu wa aina tatu, Aedes ambao ni weusi wenye madoadoa wanaosababisha ugonjwa wa dengue, Anopheles waoambukiza Malaria na Culex wanaoambukiza matende na mabusha,” amesema.
Amesema taasisi zinazofanya utafiti zinapaswa kuongeza bidii kwenye eneo hilo ili yanapotokea mabadiliko iwe rahisi kuyadhibiti.
“Tumeweka msisitizo kwenye neti na kunyunyizia dawa ndani ya nyumba, inawezekana tunafanya hatua zote hizi lakini mbu wanakaa nje. Tunahisi mbu wanakaa ndani kumbe wapo nje kwa hiyo chandalua inakuwa haina tija kama mbu anauma mchana,” amesema Dk Ndungulile.
Pia Soma
- Mavunde awatoa hofu wakazi wa Mjimwema mkoani Dodoma
- VIDEO: Makamba: Kikwete alinivutia kuingia katika siasa
- Taasisi zilizosajiliwa kama kampuni na kutekeleza majukumu ya NGO, kuanza usajili upya leo
- Chakachaka atua tamasha la ZIFF
“Taasisi zifanye tafiti kuangalia tabia za mbu na dawa zinazotumika sasa hivi zina tija, je mbu hawa hawana usugu wa hizi dawa,” amehoji.
Akizungumzia ugonjwa wa dengue bila kutaja takwimu, Ndugulile amesema maambukizi yameendelea kushuka na kuwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo.