Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbinu za kumsaidia mtoto aliyefanyiwa ukatili wa kingono

31092 Pic+ngono TanzaniaWeb

Wed, 12 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tunafahamu lipo ongezeko kubwa la idadi ya watoto wanaofanyiwa ukatili wa kingono hapa nchini. Aidha, tunaelewa wengi wa watoto hawa wanaoathiriwa na vitendo hivi vya kikatili hawana ujasiri wa kusema wazi na pengine ndio maana ni vigumu kupata takwimu rasmi. Hata hivyo, katika utafiti mmoja uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Ustawi wa Watoto (UNICEF) mwaka 2011, kati ya watoto kumi, watatu wameshawahi kukabiliwa na vitendo vya udhalilishaji wa kingono. Hali inaweza kuwa mbaya zaidi.

Mojawapo ya njia za kupata ufumbuzi wa tatizo hili, ni sisi wazazi, walimu na watu wenye nia ya kukabiliana na janga hili kujifunza viashiria vya mtoto anayepitia kipindi hiki kigumu. Baadhi ya dalili hizo ni woga usio wa kawaida dhidi ya baadhi ya maeneo, watu na hata vitu; kuwachukia baadhi ya watu bila sababu zinazofahamika wazi; mabadiliko ya tabia kama vile kujistukia, kujichukia na kukosa ujasiri anapokuwa na watu wengine.

Ni vizuri kufahamu kuwa mtoto aliyefanyiwa ukatili wa kingono hupoteza imani na watu. Kuingiliwa kimwili na mtu aliyekuwa anamwamini humfanya ajisikie kusalitiwa na matokeo yake yanaweza kuwa ni kukosa imani na mtu yeyote. Mara nyingi hutokea kila atakayejaribu kumkaribia mtoto aliyedhalilishwa anaweza kuishia kuonekana naye ni wale wale. Kwa hiyo hatua ya kwanza katika jitihada za kumsaidia mtoto aliyefanyiwa ukatili wa kingono ni kurejesha imani yake kwa watu. Lazima awepo mtu ambaye mtoto anaweza kujisikia kuwa huru kuzungumza naye.

Ili hili liwezekane, ni muhimu kushughulikia hatia na majuto anayojisikia mtoto. Hii si kazi rahisi na wengi wetu hatuiwezi kwa sababu mara nyingi tunaposikia masimulizi ya kusikitisha, mwitikio wetu wa kwanza ni kuhukumu na kulaumu. Tunapofanya hivyo, mtoto anajisikia kubebeshwa lawama na hivyo anaona bora kujichimbia handaki lake mwenyewe ajifiche humo mambo yasifahamike.

Epuka kuzungumza maneno yanayoweza kutafsirika kama lawama kwa mtoto. Unapomwambia, kwa mfano, angesema mapema haya yote yasingempata anachokisikia yeye ni lawama.

Wakati mwingine hatia anayojisikia mtoto hutokana na mawazo kuwa ukatili aliotendewa umeshaharibu maisha yake. Usimfanye akaamini wazo hilo. Mhakikishie kuwa maisha yake hayajaharibika kama anavyofikiri. Ipo mifano mingi ya wanawake maarufu duniani waliofanikiwa lakini waliwahi kuwa wahanga wa vitendo vya udhalilishaji wa kingono. Mifano ya mtangazaji maarufu Oprah Winfrey na mhubiri Joyce Mayer inaweza kumsaidia mtoto kuwa na matumaini na maisha na hiyo itapunguza majuto ndani yake.

Lakini pia, msaidie mtoto kurejesha ujasiri wake kama watoto wengine. Kudhalilishwa kunamfanya awe na mtazamo hasi na maisha yake na kujiona kama mtu duni asiyefaa kwa lolote. Wajibu wako kama mzazi, mlezi au mwalimu ni kumhakikishia kuwa pamoja na yote yaliyompata, bado yeye ni mtu wa thamani.



Chanzo: mwananchi.co.tz