Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbinu za kubaini samaki waliovuliwa kwa mabomu

50184 Pic+samaki

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Licha ya kufanya biashara ya samaki jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka minane sasa, Halima Nyundo ana siri moja aliyoificha kwa wateja wake.

Pamoja na kwamba hujitahidi kutafuta vitoweo bora kukidhi mahitaji ya wateja wake, Halima (49) hawezi kuwasaidia wateja wake kutofautisha samaki waliovuliwa kwa mabomu na wale waliovuliwa kwa njia ya kawaida.

“Mimi huwa siwezi kabisa kuwatambua samaki wanaovuliwa kwa mabomu,” anasema Halima ambaye huuza samaki wa rejareja Vijibweni katika wilaya ya Kigamboni jijini hapa.

Halima ni miongoni mwa wachuuzi na walaji wa samaki nchini ambao hushindwa kubaini sifa za samaki halali na wale waliovuliwa kwa njia haramu zikiwamo za mabomu, jambo linalofanya wawe hatarini kula vitoweo vyenye athari kiafya.

Uchunguzi wa Nukta umebaini kuwa licha ya mamlaka kupunguza uvuvi wa mabomu katika ukanda wa pwani kwa asilimia 85, baadhi ya wachuuzi wenye uzoefu wa miaka mingi katika biashara hiyo kama Halima na walaji wana tatizo la kubaini samaki waliovuliwa kwa mbinu hiyo.

Uvuvi haramu wa kutumia mabomu au baruti hutumika na wavuvi ili kurahisisha upatikanaji wa samaki wengi bila kujali madhara yatakayojitokeza kwa walaji, viumbe bahari na mazingira.

Katika uvuvi huo, vilipuzi vya kisasa vilivyotengenezwa kiwandani au vya kienyeji kama mafuta ya petroli ambayo huchanganywa na mbolea katika chupa ya plastiki yenye utambi hulipuliwa baharini ili kupata samaki wengi.

Wavuvi hao haramu huigonga miamba iliyoficha samaki kwa kitu kigumu na huwalipua na mabomu hayo mara baada tu ya kutawanyika.

Wataalamu wanaeleza kuwa kemikali zinazotumika kutengeneza mabomu hayo zina athari kubwa kwa viumbe waliopo baharini na walaji wa samaki, vilevile huharibu makazi ya samaki na mazalia yaliyopo baharini na kusabisha viumbe hao kuhama na baadhi ya samaki kutoweka.

“Nikiangalia samaki nawaona wote sawa tu. Kutambua waliovuliwa kwa njia ya mabomu kama watakuwepo sokoni ni ngumu sana ila Mungu anatuepusha,” anasema Annamaria Kiame (37), ambaye ni miongoni mwa wamiliki wa maduka makubwa ya samaki Kariakoo.

Mkazi wa Vijibweni, Sharifa Mohammed (34) anasema pamoja na kuwa aliwahi kununua samaki kipindi ambacho kulikuwa na samaki wengi waliovuliwa kwa mabomu bado inamuwia vigumu kubainisha tofauti na wale halali.

“Kipindi cha uvuvi haramu, walikuwa wanapatikana samaki wengi ila kwa sasa ni wachache na siwezi kuwatofautisha,” anasema Sharifa.

Baadhi ya walaji ambao hupata tabu kutofautisha samaki hao waliamua kupunguza kula kitoweo hicho muhimu kwa afya wakihofia kuwa huenda wangeuziwa waliovuliwa kwa mabomu ama sumu.

“Mimi ndiyo maana huwa sipendi kula samaki,” anasema Nelson Macha mkazi wa Kariakoo jijini hapa akionesha kukata tamaa.

Licha ya baadhi ya wachuuzi na walaji kushindwa kutambua samaki waliovuliwa kwa mabomu wapo wengine wenye uwezo huo licha ya kuwa hutumia njia za kienyeji kama ladha na mwonekano wa samaki.

Watalaamu hawashauri kutumia ladha kama kipimo kwa kuwa hufanywa baada ya mtu kula samaki jambo linaloweza kuhatarisha afya yake.

Mbinu za kutambua samaki aliyevuliwa kwa mabomu

Mwajuma Mpendu (42) ambaye amekuwa akiuza samaki kwa miaka minne sasa anasema njia za awali za utambuzi wa samaki waliovuliwa ni pamoja na ulegevu.

“Wanakuwa wamelegea na hata ukiwakaanga wanakuwa wachungu,” anasema Mpendu.

Ukiachana na utambuzi wa kiasili, Ofisa Uvuvi Msaidizi wa Soko la Kimataifa la Samaki la Ferry, Ahmed Mbarouk (39) anasema samaki waliovuliwa kwa vilipuzi hubadilika rangi kama alikuwa mwekundu hubadilika na kuwa wa bluu.

“Ukijaribu kumbonyeza kwa kidole hudidimia na kuacha alama ya kidole hicho kwenye samaki,” anasema Mbarouk.

Mbarouk anasema tangu ameanza kufanya kazi katika soko hilo mwaka 2014 amekuta elimu ikitolewa kwa wavuvi na wananchi na bado wanaendelea kutoa elimu kuhusu masuala ya uvuvi haramu kwa watu na njia za kuwatambua samaki waliovuliwa kwa mabomu.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayesomea masuala ya sayansi ya viumbe bahari, Kaijage Laurian anasema “samaki anakua na macho mekundu kwa kuwa mlipuko unasababisha damu kuvilia machoni”.

“Pia, anakua amelegea kwa sababu mlipuko wa bomu unavunja mifupa hasa uti wa mgongo,” anasema Laurian ambaye ameshiriki katika moja ya miradi ya kukabiliana na uvuvi haramu baharini.

Baadhi ya wavuvi hao hutumia vilipuzi bila ya kujua mchanganyiko wa kemikali zilizopo ndani ya vifaa ambavyo wataalamu wanaeleza kuwa vina athari kubwa kwa viumbe bahari na wanadamu.

Kitabu cha mbinu za kubaini uwepo wa vilipuzi (Existing and Potential Standoff Explosives Detection Techniques) kilichochapishwa na Baraza la Utafiti la Wanataaluma wa Marekani (NAS) mwaka 2004 kinaeleza kuwa vilipuzi vingi hutengenezwa na kemikali zinazojumuisha Naitrojeni (Nitrogen), Amonia (Ammonium), risasi (Lead) na unga mweusi (black powder) ambao hutengenezwa na Salfa (Sulphur) na makaa ya mawe. Mafuta ya petroli yanayotumiwa na wavuvi wa kienyeji katika vilipuzi vyao nayo hujumuisha kemikali ya zebaki (mercury) ambayo mtandao wa Live Science, unasema ni hatarishi kwa samaki na mlaji kwa kuwa husababisha magojwa licha ya kuwa madhara yake huchukua miezi hadi miaka kutokea.

“Kwa wajawazito wakila sumu ya zebaki kumsabababishia mimba kuharibika,” anasema Mtaalamu wa lishe, Debora Esau kutoka taasisi inayojihusisha na masuala ya lishe ya Panita. Mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la COSITA la mkoani Manyara, Filibert Mwakilambo anasema ulaji wa samaki waliovuliwa kwa njia za mabomu unaweza kuleta tatizo la kukakamaa kwa misuli na matatizo ya upumuaji kwa watu wenye pumu.



Chanzo: mwananchi.co.tz