Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mazoezi kwa wanaoishi na VVU

62775 MAZOEZ+PIC

Sat, 15 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tofauti na mgonjwa mwenye Virusi vya Ukimwi (VVU) ambaye yuko mahututi kitandani, ieleweke kuwa mtu ambaye anaishi na VVU akiwa mwenye afya njema anaweza kufanya mazoezi kama watu wengine ili kujenga afya ya mwili.

Ingawa ni kweli kabisa mtu anayeishi na VVU mazoezi yake anayotakiwa kufanya huwa na tofauti ndogo sana na asiye na maambukizi.

Mwenye maambukizi ya VVU kama walivyo wengine, atahitajika kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi mepesi mara kwa mara katika maisha yake.

Atahitajika kufanya mazoezi ya kiasi yasiyo magumu yanavyojulikana Aerobics Exercises.

Sababu ya kutakiwa kufanya mazoezi haya ni kwa sababu mazoezi hayauchoshi mwili na hutumia kiasi cha wastani cha nishati ya mwili kulinganisha na mazoezi magumu Anaerobics Exercises.

Ikumbukwe kuwa mtu anayeishi na VVU hutakiwa kutunza kiasi cha nishati kilichopo mwilini mwake kwa kuwa anahitaji nishati hiyo kwa ajili ya mambo muhimu ikiwamo kujenga mwili na kinga imara.

Pia Soma

Mazoezi mepesi ambayo mtu mwenye VVU anashauriwa kuyafanya ni pamoja na kutembea, kukimbia kidogo kidogo, kuruka kamba, kuogelea, kuendesha baiskeli na kucheza muziki wa harakaharaka.

Mazoezi mengine anayoweza kuchanganya na hayo ni pamoja na mazoezi ya viungo ikiwamo kupasha mwili moto na kunyoosha misuli na kunyanyua vitu vyenye uzito wa wastani kwa ajili ya kujenga misuli.

Mazoezi mengine yanayowafaa zaidi watu wazima wanaoishi na VVU ni zoezi la Yoga yenye asili ya nchini India ambayo ni rahisi kujifunza na kulifanya na linafaida lukuki kiafya.

Mazoezi haya yote yanafaida mbalimbali kwa mtu anayeishi na VVU ikiwamo kuimarisha afya ya moyo na mapafu, kujenga misuli imara ya mwili, kuondoa taka mwili kwa njia ya jasho, kudhibiti uzito wa mwili kwa kupunguza mrundikano wa mafuta mwilini.

Faida zingine ni kujenga kinga imara, kumpa burudani na kumpa furaha, kulala usingizi mnono na kumuepusha na magonjwa ya akili ikiwamo msongo wa mawazo na sonana.

Vile vile mazoezi haya yanamuepusha na vishawishi vinavyoweza kumuingiza katika suala la kujamiiana na wenza wapya na matumizi ya vilevi.

Mazoezi mepesi ni salama kwa mtu ambaye anaishi na VVU na yanaweza kufanyika nusu saa (dakika 30) kwa siku katika siku tano za wiki.

Ili kuwa salama na mazoezi haya atahitajika kula mlo kamili uliozingatia kanuni za afya pamoja na kuwa na utamaduni wa kunywa maji mengi angalau kwa siku glasi 10 au lita 1.5-3 kwa siku.

Inashauriwa kwa anayeishi na VVU kufanya mazoezi mepesi endapo tu hana dalili zozote za kuumwa na pia inashauriwa kuhudhuria kliniki kama anavyopangiwa.

Mwandishi wa makala haya ni daktari wa binadamu

Chanzo: mwananchi.co.tz