Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Maziwa ya mbuzi huwasaidia wenye vidonda vya tumbo’

0463f06d6d12d30c6c916f3a08c5a7e6 ‘Maziwa ya mbuzi huwasaidia wenye vidonda vya tumbo’

Wed, 16 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAZIWA ya mbuzi husaidia kwa kiwango kikubwa kutibu vidonda vya tumbo; utafiti umebaini.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (Taliri), hali hiyo inatokana na maziwa ya mbuzi kuwa na virutubisho vinavyosaidia kutibu ugonjwa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea kituo cha TALIRI kilichopo jijini Tanga, Mtafiti Mwandamizi wa Mifugo kutoka Taliri, Walter Mangesho, alisema katika utafiti huo walifanya majaribio kwa maziwa ya ng’ombe, lakini maziwa ya mbuzi yaliyotoa matokeo mazuri zaidi.

Alisema hali hiyo inatokana na maziwa ya mbuzi kuwa na virutubisho vinavyohitajika ili kuzalisha kwa wingi kinga katika mwili wa binadamu.

"Tumebaini kuwa maziwa ya mbuzi ambaye amelishwa vizuri ni tiba nzuri na ya uhakika yanaweza kutibu kabisa ugonjwa wa vidonda vya tumbo na hivyo, niwaombe wananchi kuzingatia tiba hiyo ili kukabili tatizo hilo," alisema Magesho.

Hata hivyo, alisema kutokana na mafanikio hayo, watu wengi wamekuwa wakifika katika kituo hicho kutoa ushuhuda wa namna maziwa hayo yalivyowasaidia kutibu matatizo ya vidonda vya tumbo, hali inayosababisha kufanya utafiti kwa kina zaidi.

"Bado tunaendelea kufanya utafiti zaidi ili kubaini kama maziwa hayo yanatibu maradhi mengine zaidi, lakini pia tunaendelea kujiridhisha kama mgonjwa anapata tiba ya kudumu," alisema.

Kuhusu malisho, alisema mbuzi wanaopata malisho mazuri na chakula bora wana uwezo wa kutoa maziwa lita mbili kwa siku na maziwa yake yana virutubisho vingi vinavyomsaidia binadamu kuongeza kinga ya mwili na kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Kwa mujibu wa mtafiti huyo, wamekuwa wakizalisha mbegu bora za mbuzi wa maziwa na sasa wamejipanga kuhakikisha wanaongeza mbegu bora ili wananchi wanunue kwa wingi na hatimaye kupata tiba ya tatizo hilo.

"Watanzania njooni mjifunze na mnunue ili mboreshe afya zenu na hata mifugo yenu iimarike," alisema Mangesho.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dk Zablon Nziku, alisema Taliri ipo kwa ajili ya kufanya tafiti zitakazowasaidia wafugaji kupata matokeo bora ya mazao yatokanayo na mifugo ili kuinua uchumi na kubadilisha dhana ya ufugaji na kuwa wa kisasa.

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja wamefanikiwa kuwafikia wafugaji 349 wa ng’ombe wa maziwa na kuwapatia teknolojia mbalimbali za ufugaji kuhusu ng’ombe wa maziwa.

Chanzo: habarileo.co.tz