Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mayai: Protini 100%, ubora afya yako kwa namna hii

Thu, 7 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tiba mifupa, nywele, kucha, sumu Macho, ubongo wazee & watoto…

MARA nyingi iko wazi hasa vijana na zaidi watoto wanapenda sana mlo mayai. Msingi wa mvuto wao uko katika ladha zaidi na hata pale wanapoangukia kwa simulizi za ‘chipsi mayai’ au ‘mayai kwa mkate’ hasa kwa jamii za Magharibi.

Ni lishe ambayo inatoka kwa kiumbe kuku zaidi na kundi la jamii ya ndege na wanaofanana nao kama vile bata.

Inapokuwa mlo, uandaaji wake unaweza kuwa wa namna nyingi, lakini kuu iko katika makundi mawili, ya kukaanga na kuchemsha, ingawaje wapo wachache wanakula hata mabichi.

SIFA ZAKE

Kwa kurejea wasifu wa kitaalamu kutoka kwa wataluma wa Farmers Market, mayai yanamsaidia mtumiaji kuhisi mwenye shibe kwa kipindi kirefu. Hiyo ni kutokana na kila yai kuwa na uwezo kumpatia malaji protini yenye ubora na virutubisho mbalimbali muhimu vinavyohitajika mwilini, isipokuwa vitamin C.

Hapo wanaeleza ndio kiini cha ushauri kwamba kila yai linapaswa kuliwa kwa kujumuishwa na walau matunda au juisi ya machungwa, pia mkate uliotayarishwa kwa unga kumwezesha mtumiaji kuwa katika hali nzuri zaidi kiafya.

Pia, ina nafasi ya kumuondolea mlaji upungufu wa madini ya chuma mwilini, pale anapohisi dalili mbalimbali za uchovu, kuumwa vichwa na kuwashwa ngozi.

Ni madini yanayobeba hewa ya oksijeni kwenye damu na hufanya kazi muhimu katika kuimarisha kinga za mwili na usanisishaji wa nishati mwilini.

Aidha, madini ya chuma yanayopatikana kwenye kiini cha yai, yako katika mfumo ulio tayari kufyonzwa na kutumika mwilini, kuliko aina ya chuma zinazopatikana kwenye virutubisho vingine vya vyakula.

Idadi ya virutubisho vilivyomo kwenye mayai, inaelezwa inayafanya kuwa na mchango muhimu kwenye lishe ya mlaji. Kuna utafiti uliofanywa baina ya walaji mayai na wasiotumia, ulibaini wasiotumia mayai wanaangukia katika upungufu mkubwa wa viinilishe; vitamini A, E na B12.

Msingi wake kitaalamu ni kwamba mayai yanachangia mwilini kiasi cha asilimia 10 hadi 20 cha madini aina ya folate na kiasi cha asilimia 20 hadi 30 cha vitamin A, E na B12 kwa watumiaji wake.

Hali kadhalika, licha ya katika miaka ya 1990 kuwapo watafiti walioitangaza vibaya kuwa na lehemu, zipo tafiti kinazani zilizofuatilia na kuyatetea mayai kwamba hayana uhusiano na ongezeko la lehemu mwilini, hata kumfikisha mlaji katika magonjwa ya moyo.

Pia, mtu anapotaka ama kudhibiti uzito wake au kuupunguza, basi mayai yana nafasi kama lishe mbadala, kwani hata utafiti mbalimbali umekuja na uthitibitisho huo kutoka kwa walaji wa mayai.

Eneo lingine la faida ya ulaji mayai, inashuhudia katika afya ya ubongo. Ni kirutubisho kinachojulikana kama choline, kinachosaidia kuboresha ubongo na hasa kwa watoto wadogo, pia wazee.

Kwa mama majamzito naye ana faida ya kirutubisho choline, kila anapokula walau yao moja kwa siku, kwani inamnufaisha kirutubisho hicho cha choline, kwa wastani wa asilimia 28.

Ni kirutubisho muhimu sana hata wakati wa mama kunyonyesha, akiba yake ya kirutubishi inapokuwa imepungua na ni wakati muhimu sana kwa ukuaji wa ubongo wa mtoto na uboreshaji wa kumbukumbu yake atakayodumu nayo.

Katika eneo la uwezekano wa mtu kupatwa na magonjwa yanayohusiana na macho, mayai tena yanachukua nafasi ya kuwa na maboresho yake.

Ulaji mzuri wa mayai, pamoja na mboga kama spinachi kwa kiasi kikubwa, ni msaada mkubwa katika kuyakinga macho, dhidi ya magonjwa ambayo vinginevyo yanamuweka mhusika pagumu.

Mayai yanaelezwa tena kwa nafasi kubwa yanapunguza madhara yanayotokana na kuchakaa mboni na lensi ya macho, ikiwamo matokeo ya umri wa mwanadamu.

Pia, imedumu kuwa chanzo muhimu cha kuondoa baadhi ya sumu mwilini (antioxidants) zinazofanya kazi muhimu ya kuhakikisha macho ya binadamu, yanadumu kuwa salama.

Vyanzo hivyo kwa kawaida, hukusanyika kwenye macho kuyalinda dhidi ya miale mikali ya mwanga, yenye madhara makubwa na hivyo, kula mayai tangu umri mdogo, ni kujihakikishia kupata virutubisho na kujiepusha na upofu.

BINGWA PROTINI

Ikiwa ni chanzo kikuu cha protini mwilini, sehemu ya aina kuu tatu ya vyakula inayojenga mwili, ikihusika kwenye ujengaji na ukarabati wa chembechembe na tishu mbalimbali za mwili. Mayai yanapewa nafasi ya bingwa wa kusambaza protini hizo muhimu mwilini.

Tindikali za amino (amino acids) ndiyo matofali yanayojenga protini hizo na kwa bahati mbaya miili ya binadamu, haina uwezo wa kuzalisha tindikali hizo, ni lazima zipatikane kupitia vyakula.

Kwa maana hiyo, kula mayai husaidia kukua kwa mwili na kutunza chembechembe hai na tishu za miili yetu. Kwa mfano, mayai, maziwa na nyama, zote ni protini zilizo kamili na bora.

Lakini, mayai yanabaki bora zaidi kwa sababu yana portini asilimia 100; maziwa asilimia 93 na nyama ya ng’ombe au samaki asilimia 75.

Inakadiriwa kitaalamu kila yai moja, lina kiwango sawa cha protini na gramu 30 za nyama ya ng’ombe, samaki au kuku iliyopikwa.

NYWELE, KUCHA, MIFUPA

Wataalamu wanaainisha kwamba ni chanzo cha vitamini D na kwa maana nyingine, ni muhimu kwa kwa madini ya calcium mwilini, ili kuimarisha afya za mifupa. Hivyo mayai na maziwa vinasaidia kuepuka tatizo la mifupa mwilini au hata udhaifu wake kuvunjika kirahisi.

Mayai husaidia kuboresha afya ya nywele na kucha kwa sababu ya kuwa na tindikali za amino zenye wingi wa madini ya salfa na wingi wa vitamini na madini mengine.

•Makala hii ni kwa mujibu wa taarifa za utaalamu wa lishe na afya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live