Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawaziri waliomaliza muda watoa ya moyoni

C18ac727aa478ee328c8f1520abc0b79 Mawaziri waliomaliza muda watoa ya moyoni

Sun, 8 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WALIOKUWA mawaziri na manaibu katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Tano, wamemshukuru Rais John Magufuli kwa kuwaamini, huku wengi wakieleza kupata somo kubwa la uongozi na utendaji bora kutoka kwake.

Wakizungumza kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya mawaziri wamemshukuru Mungu kuwawezesha kuhitimisha majukumu salama na kumshukuru Magufuli alivyokuwa mwalimu mwema na bora wa kufanya kazi kwa kasi kubwa, uadilifu na uthubutu.

Baadhi wameshauri watakaoteuliwa uwaziri/unaibu waziri katika kipindi kingine, watambue kuwa wameaminika, hivyo wawe msaada katika utendaji wa serikali na kupaisha nchi kimaendeleo.

Washukuru Mungu, Magufuli

“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuhitimisha salama uwaziri…Asante sana Rais Magufuli. Hakika Nimejifunza mengi kutoka kwako. Umenifanya kusimama imara wakati wote kulinda maslahi ya Tanzania na watanzania," alisema aliyekuwa Waziri wa Afya, Maendeo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Alisema, “Naamini wengi watakubaliana nami kuwa sekta ya afya ni moja ya sekta ambazo zimepata mafanikio makubwa katika kipindi hiki cha utawala wa awamu ya tano, hatua iliyotokana na utashi na dhamira ya dhati ya Rais Magufuli ya kutaka kuboresha maisha ya watanzania hususan wa kipato cha chini.”

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alimshukuru Mungu kwa kumwezesha kumaliza kuwatumia Watanzania kwa mafanikio katika sekta kilimo.

Alimshukuru Rais Magufuli kwa kumwamini kipindi chote, ushirikiano mkubwa aliompatia na kumuwezesha kutekeleza majukumu . Alisema aliwashika mawaziri wake mkono na kuwasaidia, hivyo watakaoteuliwa watakuwa na uwezo wa kuendeleza yaliyoachwa, kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi.

Wamejifunza mengi

“Nimejifunza katika kipindi chake chote cha uongozi kuwa nchi yoyote ili iweze kuwa na mafanikio makubwa lazima iwe na kiongozi shupavu na mwenye maono…Ukiwa na kiongozi mwenye maono, mwenye hekima na mwenye uwezo wa kutenda lazima mtakuwa na mafanikio,” alisema Hasunga.

Kwa upande wake, aliyekuwa Naibu Waziri, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Dk Anjelina Mabula alishukuru kwa kumaliza salama kutumikia Serikali ya Awamu ya Tano kwa kipindi cha miaka mitano bila tatizo.

Pia alimshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini kwa kipindi chote na kumpa mwongozo katika kazi na kumfanya atumikie vizuri taifa..

“Ni jambo la kujivunia na kumshukuru Mungu kumpata Rais ambaye ni mwenye maono na msimamo,” alisema.

Dk Mabula alisema katika kipindi chote cha uongozi wa Magufuli, amejifunza kuwa usimamizi, ufuatiliaji, kujiamini na kuacha kufanya kazi kwa mazoea, kuna tija katika uongozi.

“Nimejifunza kwamba mtu anapopanga kufanya jambo fulani na akaamini linaweza kutendeka na kuleta matokeo chanya, hana budi kulisimamia mpaka likatendeka,” alisema .

Alisema maeneo yote ambayo Magufuli alisimamia, mambo yamekwenda vizuri ikiwemo eneo la makusanyo ya mapato. Alitoa mfano wa sekta ya ardhi na kusema zamani ulipaji kodi, ulionekana kuwa jambo lisilowezekana.

Kwa mujibu wa Dk Mabula, kutokana na usimamizi mzuri, ulipaji wa kodi hizo ulipanda kutoka Sh bilioni 50 hadi Sh bilioni 200. “Ni kitu kinachowezekana. Ni suala la usimamizi, ufuatiliaji na kujiamini na kuacha kuendekeza suala la mazoea,” alisema.

Mawaziri watarajiwa

Alishauri watakaochaguliwa akisema, “Sasa ukichaguliwa ujue umepewa dhamana ambayo unatakiwa uitumike na watanzania waone kweli unatumika. Hasa katika usimamizi, ufuatiliaji na kutoka ofisini.”

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alimshuru Mungu kwa kumaliza salama na kumshukuru Magufuli kwa kumwamini. Pia alieleza funzo alilopata katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.

“Kwa kweli nimejifunza, maelekezo, dhamira na kiu ya rais ni kuona Tanzania inakua kupitia viwanda. Na alitumia sekta ya nishati kama kichocheo cha ukuaji huo wa viwanda,” alisema. Subira alisema anatarajia mawaziri wajao, wataendeleza waliyoyaacha ikiwamo usambazaji umeme.

Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, pia alisema amejifunza mambo makubwa manne kutoka kwa Magufuli ambayo ni kuonesha njia, kujituma, kutumikia na kuwajibika.

Walioanza na kuhitimisha na JPM

Rais John Magufuli alitangaza baraza lake la kwanza la mawaziri Desemba 10, 2015 ikiwa ni mwezi na siku tano tangu alipoapishwa Novemba 5, 2015 jijini Dar es Salaam.

Aliteua na kuwatangaza mawaziri na manaibu waziri 28 siku ya kwanza ya kuunda baraza lake la kwanza, lililokuwa na mawaziri 19 huku wizara zikiwa 18. Nafasi nne za uwaziri zilibaki wazi hadi alipozijaza Desemba 23, ikiwa ni siku 13 tangu alipotangaza baraza.

Desemba 23, 2015 Magufuli alikamilisha baraza lake, kwa kujaza nafasi za uteuzi wa mawaziri alizobakiza.

Oktoba 2017, Rais Magufuli alifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri kwa kugawanya Wizara ya Kilimo na Mifugo na Wizara Nishati na Madini na kuongeza wizara mpya mbili na kufikisha jumla ya wizara 21 .

Walioanza na JPM

Kati ya mawaziri na manaibu 32 walioanza na Rais John Magufuli kupitia uteuzi aliofanya kwa awamu mbili mwaka 2015, 19 ndio wamehitimisha salama safari ya miaka mitano ya kuongoza wizara mbalimbali huku mmoja akiwa ameteuliwa ubalozi. Mwingine alifariki dunia Mei mwaka huu na wengine walienguliwa kwa sababu mbalimbali za kiutendaji.

Mei mwaka huu baraza la mawaziri lilipata pigo kwa kuondokewa na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Augustine Mahiga ambaye alikuwa miongoni mwa wateule wa kwanza akiwa Waziri wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi Vijana, Ajira na Walemavu, Dk Abdallah Possi ni miongoni mwa wateuliwa wa kwanza ambaye mwaka 2017 Magufuli alimteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani.

Miongoni mwa mawaziri na manaibu 17 walioanza na kuhitimisha salama majukumu yao, 10 walidumu wizara moja bila kuhamishwa hadi Novemba 5, 2020, wadhifa wao ulipokoma baada ya Rais Magufuli kuapishwa kuongoza kipindi kingine.

Waliohitimisha safari

Mawaziri na manaibu walioanza kazi na Rais Magufuli na kuhitimisha safari salama ni Angella Kairuki alikuwa Waziri wa Utumishi na Utawala Bora na kuhitimisha akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji; William Ole Nasha alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia); Dk Medard Kalemani alikuwa Naibu Waziri Wizara ya Nishati na Madini (Waziri wa Nishati)

Dk Harrison Mwakyembe alianzia Waziri wa Katiba na Sheria na kuhitimisha akiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Stella Manyanya aliteuliwa kuwa Naibu Waziri, Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi na kumaliza akiwa Naibu wa Viwanda na Biashara.

Profesa Makame Mnyaa Mbarawa aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na kuhitimisha akiwa Waziri wa Maji . Isack Kamwelwe alikuwa Naibu Waziri wa Maji na amehitimisha akiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Luhaga Mpina aliteuliwa kwa mara ya kwanza Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira amehitimisha kazi akiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Waliodumu wizara moja

Wengine waliomaliza salama bila kuhamishwa wizara ni Dk Philip Mpango aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango na Profesa Joyce Ndalichako aliyekuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.

Dk Hussein Mwinyi alishika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) tangu mwanzo hadi alipohitimisha kwa kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar. Wengine na wizara walizoongoza kwenye mabano ni Jenista Mhagama (Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi Vijana, Ajira na Walemavu); William Lukuvi (Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi); Dk Angelina Mabula (Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) na Ummy Mwalimu (Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) .

Wengine ni Ashatu Kijaji aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Hamad Masauni alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Anthony Mavunde alikuwa Naibu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi Vijana, Ajira na Walemavu na Suleiman Jafo aliyeanza akiwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi na kuhitimisha akiwa waziri wa wizara hiyo.

Waliopumzishwa, wakarejeshwa

Kati ya mawaziri na manaibu hao walioanza na Magufuli, wapo waliojikuta wakipumzishwa kwa sababu za kiutendaji na baadaye wakarejeshwa na wakawa sehemu ya waliohitimisha utumishi wao salama.

Mawaziri hao ni Dk Mwigulu Nchemba alikuwa Waziri wa Kilimo na baadaye akawa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi; wadhifa uliotenguliwa Mei 2018 na kisha Mei mwaka huu Rais Magufuli alimteua kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

George Simbachawene amehitimisha akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, wadhifa alioteuliwa Januari mwaka huu. Awali, alipotangaza baraza, Magufuli alimteua Simbachawene kuwa Waziri Ofisi ya RaisTamisemi wadhifa aliojiuzulu Septemba 2017.

Julai 2019, Magufuli alimrejesha katika baraza la mawaziri kwa kumteua kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano kabla ya Januari mwaka huu kumteua kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Walioenguliwa

Wateule wengine wa uwaziri na unaibu ambao uteuzi wao ulitenguliwa na wizara walizokuwa wamepangiwa awali ni: Januari Makamba (Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira), Edwin Ngonyani ( Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Profesa Sospeter Muhongo (Wizara ya Nishati na Madini), Susan Kolimba (Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki).

Wengine ni Charles Kitwanga (Waziri wa Mambo ya Ndani), Ramol Makani (Naibu Waziri wa Maliasi na Utalii), Charles Mwijage (Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji), Nape Nnauye (Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo) na Anastazia Wambura (Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo).

Profesa Jumanne Maghembe aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na Gerson Lwenge aliyekuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, pia walienguliwa njiani.

Habari hii imeandikwa na Stella Nyemenohi na Halima Mlacha

Chanzo: habarileo.co.tz