Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawaziri 13 wanawake wanaopambana na corona Afrika

102343 Pic+wanawake Mawaziri 13 wanawake wanaopambana na corona Afrika

Tue, 14 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Duniani kote, ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona, umekuwa janga la kufanya sayari hii kusimamisha shughuli nyingi za kibinadamu lakini umeibua ushindani wa uwezo wa uwajibikaji kwa viongozi wa kisiasa.

Kwa Afrika habari za ugonjwa huu zimeanza kuibuka zaidi mwezi uliopita, na serikali zake zinapambana katika kuhakikisha hausambai zaidi kama ilivyo bara la Ulaya na Asia.

Takwimu za kidunia zinaonyesha mpaka kufikia jana duniani vifo vilivyotokana na COVID-19 vilifikia 110,075 huku watu 1,797,512 wakiambukizwa na wengine 412,129 walishapona ugonjwa huo.

Watu 750 wamefariki barani Afrika kufuatia ugonjwa huo na idadi ya waliokwisha kuambukizwa ikifikia 14,384 na 2,496 wamepona.

Katika kada za uongozi, wizara ya afya ndiyo mama katika kupambana na janga hili lililoikumba dunia, hata hivyo kitu cha kipekee ni uwezo wa kupambana walionao mawaziri wanawake barani Afrika ambao kinyume na matarajio wameonekana kuwajibika ipasavyo.

Wameonyesha uwezo mkubwa katika kuhakikisha kwamba wanakuwa bega kwa bega na wataalamu kwa kuwapa sapoti madaktari, wauguzi na watumishi wengine wa afya katika nchi zao kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma na washukiwa wanachunguzwa huku wakitoa elimu ya kujikinga na taarifa rasmi za ugonjwa wa corona.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Kati ya nchi 51 za Afrika kuna mawaziri wanawake 13 wanaosimamia wizara za afya. Kati yao tisa ni madaktari waliosomea na wengine waliteuliwa kushika wadhifa huo kulingana na nafasi walizokuwa nazo kisiasa na historia zao.

Nchi zilizobarikiwa kuwa na mawaziri wa afya wanawake ni pamoja na Angola, Burkina Faso, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Misri, Eritrea, Ethiopia, Eswatini. Guinea Bissau, Liberia, Msumbiji, Somalia, Uganda na Tanzania.

Mwananchi linakuletea orodha yao na dondoo kadhaa kuwahusu na nyadhifa mbalimbali walizowahi kushika kabla ya kuongoza wizara hiyo.

Ummy Ally Mwalimu – Tanzania

Ni mbunge wa Viti Maalum kutoka chama tawala CCM, ameshika nyadhifa ya kuwa Waziri wa Afya tangu mwaka 2015 alipoteuliwa na Rais John Magufuli na amekaa vipindi viwili bungeni.

Ummy ambaye ni mwanasheria pia ana shahada ya uzamili katika sheria kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria aliyoipata mwaka 2001. Kati ya mwaka 2000 na 2010 amekuwa akifanya kazi katika mashirika mbalimbali ya serikali na yasiyo ya serikali yanayohusika na masuala ya sheria, utafiti na utawala.

Katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete amewahi kusimamia wizara kadhaa katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2014 alikuwa naibu waziri wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Pia amewahi kuwa naibu waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Sheria na Katiba.

Mwaka 2015, Rais Magufuli alimteua kuwa Waziri wa Afya nafasi aliyoweza kuitumikia vilivyo na kuwa miongoni mwa mawaziri wachache waliodumu katika wizara tangu uteuzi wa awali.

Akiwa Waziri wa Afya amefanya mambo mengi ikiwemo kuzuia mimba na ndoa za utotoni kwa kupelekwa muswada bungeni na baadaye kuwa sheria. Mbali na hayo ameonyesha juhudi katika mambo mengi ikiwemo kuhakikisha anaweka nguvu katika kutokomeza vifo vya mama na mtoto.

Dk Jane Aceng – Uganda

Kitaaluma ni daktari bingwa wa magonjwa ya watoto lakini pia mwanasiasa nchini Uganda. Ni Waziri wa Afya katika Bunge la Uganda. Aliteuliwa kushika wadhifa huo Juni 6 mwaka 2016.

Kabla ya hapo, Juni mwaka 2011 mpaka Juni 2016 alikuwa Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu katika Wizara ya Afya nchini humo.

Dk Aceng ana shahada ya udaktari na shahada ya upasuaji lakini pia ana shahada ya uzamili ya udaktari wa watoto na shahada ya uzamili ya udaktari zote alizipata kutoka Chuo Kikuu cha Afya Kishiriki cha Makerere.

Lakini pia ana stashahada ya uongozi na utawala kutoka Uganda Management Institute.

Nyota yake iling’ara tangu akiwa Wizara ya Afya alipoteuliwa kuwa mkurugenzi mkuu wa huduma za madawa lakini pia ameshawahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Lira.

Amna Nurhusein - Eritrea

Aliteuliwa kushika wadhifa huo mwaka 2009. Kabla ya hapo ameshika nyadhifa nyingi ikiwemo ya waziri wa wizara ya utalii.

Dk Fawziya Abikar - Somalia

Dk Abikar ameshika wadhifa huo kwa kipindi sasa na amekuwa mstari wa mbele katika kuonyesha jitihada zake katika kupambana na ugonjwa wa Covid19 akisaidiana na jopo la wataalamu wengine.

Dk Hala Zayed- Misri

Dk Zayed amekuwa akiongoza kama Rais wa shule ya sayansi ya tiba, akiongoza tume ya kupambana na rushwa, lakini pia ni Waziri wa Afya na idadi ya watu nchini humo.

Pia ameshika nyadhifa nyingine nyingi kama mkurugenzi mkuu wa kitengo cha hospitali katika wizara hiyo, mkuu wa kitengo cha utawala cha ufuatiliaji na mkuu wa kitengo cha mikopo katika wizara hiyo.

Ana elimu ya shahada ya uzamili ya udaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi na udaktari (PHD) na shahada ya uzamili katika utawala.

Dk Jacqueline Lydia Mikolo–DRC

Ameongoza wizara hiyo tangu Mei 6, 2016. Aliwahi kuwa mkuu kitengo cha usimamizi wa manunuzi ya umma katika idara ya kazi.

Katika mkutano wa 69 wa Shirika la Afya Duniani (WHO), uliofanyika Mei 23–28 huko Geneva, Uswisi alisimulia namna nchi hiyo ilivyopiga hatua katika mapambano ya maradhi na mipango iliyojiwekea kwa kipindi cha mwaka 2016-2021.

Dk Leonie Claudine Sorgho/Lougue– Burkina Faso

Yeye ni daktari bingwa wa vipimo vya radiolojia na pia ni mkufunzi/profesa katika chuo kikuu anayetoa elimu ya radiolojia lakini pia ni mtaalamu wa ugunduzi wa magonjwa mbalimbali kupitia mashine za radiolojia.

Alishawahi kuwa mkurugenzi wa mafunzo na utafiti katika kitengo nyeti katika chuo kikuu cha Ouaga I Joseph KI-ZEBRO kilichopo Burkina Faso mwaka 2015 hadi 2019.

Dk Lia Tadesse Gebremedhin – Ethiopia

Dk Lia amewahi kuwa mkurugenzi mtendaji kitengo cha mafunzo ya afya ya uzazi katika Chuo Kikuu cha Michigan. Pia amewahi kufanya kazi kama mkurugenzi wa mradi wa mama na mtoto kupitia Shirika la Jhpiego nchini Ethiopia.

Alipata elimu yake ya udaktari na ubobezi katika Chuo Kikuu cha Jimma na pia Addis Ababa, Ethiopia.

Lizzie Nkosi – Eswatini

Kati ya mawaziri wanawake wanaofanya vizuri katika nchi hiyo ndogo kabisa barani Afrika, Lizzie ni mmojawapo. Japokuwa nchi hiyo bado haijapata maambukizi ya corona ameweza kufanya matayarisho ya kutoa elimu sahihi kwa wananchi na wataalamu wa afya.

Maria Inacia Co Sanha – Guinea Bissau

Maria alihitimu elimu yake huko Ureno, alishawahi kushika vitengo nyeti katika wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya afya na wizara ya kazi na huduma za jamii nchini humo.

Dk Nazira Abdula – Msumbiji

Yeye ni mtaalamu na daktari bingwa wa magonjwa ya watoto, alihitimu katika Chuo cha Hospitali ya Maputo baada ya kupata elimu yake huko Ureno.

Dk Nazira pia ana shahada ya uzamili katika masuala ya lishe na mpangilio wa chakula.

Kabla ya kuwa waziri alishika nyadhifa mbalimbali ikiwemo naibu waziri wa wizara hiyo kwa mwaka 2010 hadi 2014 na amekuwa waziri wa afya tangu mwaka 2015.

Dk Silvia Lutucuta – Angola

Ni mtaalamu wa fizikia, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na profesa/ mkufunzi wa chuo kikuu, pia ni mkuu wa kitengo cha utafiti katika shule ya tiba na amewahi kushiriki katika tafiti nyingi zikiwemo zihusuzo magonjwa ya moyo.

Akiwa na miaka 16 alishaingia kusomea utaalamu wa tiba na miaka sita baadaye alihitimu masomo yake mwaka 1990 akiwa ni mwanafunzi mdogo na bora kuliko wote akiwa na umri wa miaka 21 alipata ufadhili wa masomo.

Amesoma katika vyuo vingi akibobea katika fani ya udaktari wa magonjwa ya moyo duniani. Alianza kufundisha akiwa na miaka 19.

Dk Wilhemina Jallah – Liberia

Dk Wilhelmina Jallah alishawahi kuwa mkuu wa kitengo cha magonjwa ya kinamama na uzazi katika kituo cha tiba cha F. Kennedy mjini Monrovia, Liberia, naye kama walivyo mawaziri wenzake wanawake hayuko nyuma katika mapambano dhidi ya virusi vya corona.

Chanzo: mwananchi.co.tz