Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawakili: Uvunaji figo, moyo isiwe biashara

7867cf0280eddf6d5685e17eb9e4652d.jpeg Mawakili: Uvunaji figo, moyo isiwe biashara

Wed, 17 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WANASHERIA wamesema muswada wa sheria wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya uvunaji wa viungo vya binadamu kama vile moyo, ini na figo uhakikishe suala hilo halifanywi kibiashara.

Waliyasema hayo jana walipozungumza na HabariLEO lilipotaka kujua ni mambo gani ya msingi yanapaswa kuzingatiwa katika muswada huo utakaosaidia kutungwa kwa sheria ya uvunaji wa viungo hivyo.

Wakili wa kujitegemea, Albert Msando, alisema sheria itakayotungwa ihakikishe suala la fedha halipewi nafasi kubwa ili uvunaji huo wa viungo vya binadamu usigeuke kuwa chanzo cha kipato au biashara.

“Suala la fedha ni muhimu lakini isiwe gharama kubwa ili watu tusianze kuwindana, au mtu anaanza kusubiri mama yake afe maana anaona anachelewa, kwa hiyo suala la gharama lazima tuliangalie ili liwe nafuu kwa watu wengi kwa sababu mpaka mtu ahitaji figo maana yake uhai wake uko hatarini, tusiruhusu kukawa na gharama kubwa halafu ikawa biashara,” alisema Msando.

Alisema sheria ni muhimu katika kuweka utaratibu maalumu kwa ajili ya suala lolote linalotakiwa kufanyika. Alisema suala la uvunaji wa viungo vya binadamu linachangamoto kutokana na mila na desturi za Kitanzania.

Msando alisema kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Jinai ni kosa kuchezea maiti kwa kuifanya kitu chochote kile hivyo kimtazamo suala la kutoa viungo lina changamoto hiyo ya mila na desturi.

“Kwa hiyo sheria inapaswa kuondoa changamoto hii ya kimtazamo kwamba unapovuna au kuchukua viungo kwa ajili ya kufanya tafiti au kwa ajili ya kutumia kwa mtu mwingine ambaye anauhitaji, lazima ufanyike kwa utaratibu ambao unaeleweka na kila mmoja wetu,” alisema Msando.

Dk Onesmo Kyauke ambaye pia ni wakili wa kujitegemea alisema sheria itakayotungwa ya uvunaji wa viungo vya binadamu isiruhusu malipo ya aina yoyote na itamke kuwa kufanya hivyo ni kosa la jinai.

Alisema sheria pia inapaswa kuweka utaratibu wa watu kukiri au kukubali kabla hawajafa au kwamba viungo vyao vitumike au ndugu wakubali kwamba viungo vya ndugu yao vitolewe, lakini siyo kwa biashara.

“Suala hili linahitaji umakini sana kwa sababu ukikosea kidogo unaweza kujikuta unafanya biashara ya viungo vya binadamu; ila sheria ni nzuri kwa maana kwamba viungo vya binadamu vinaweza vikaokoa binadamu wengine ambao wanahitaji,”alisema Dk Kyauke.

Wakili mwingine wa kujitegemea, Onesmo Mpinzile alisema ni vyema sheria itakayotungwa ieleze kama kutakuwa na fedha, na fedha hiyo inapotolewa iende wapi na kufanya kazi gani.

Alisema sheria itamke kama fedha hiyo itaenda kwenye mfuko maalumu au kwa ndugu wa marehemu aliyetoa viungo.

Mpinzile alisema sheria hiyo inatakiwa kutoa nafasi kwa mgonjwa kuamua viungo vyake ama vitumike kwa fedha na fedha hiyo iende wapi au vitumike kama sehemu ya sadaka yake kwa watu wengine wanaohitaji viungo, hivyo sheria lazima iweke mfumo mzuri wa usimamizi na kulinda matakwa ya marehemu.

“Ni vyema sheria izingatie matakwa ya marehemu kwamba alisema nini kabla ya kufa au ndugu waseme marehemu alipenda mwili au sehemu ya mwili wake itolewe kwa ajili ya utafiti au kukokoa maisha ya watu wengine,” alisema.

Reuben Simwanza alisema fedha ni suala lisilokwepeka japo umakini unatakiwa kwa sababu kuna mambo mengi ya kuzingatiwa ikiwemo utimamu wa akili ya mgonjwa, afya na utimamu wa mawazo au uhuru wa mawazo yake.

Chanzo: www.habarileo.co.tz