Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maumivu sugu ya miguu kwa mwanamichezo

48543 Dk+Shita+Samwel

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kwa mwanamichezo kila kinachofanyika wakati wa mazoezi ni lazima eneo la mguu litahusika na mambo mbalimbali ikiwamo kuruka, kukimbia na kutembea.

Matendo haya ndiyo yanachangia majeraha ya mara kwa mara eneo la chini ya mguu ikiwamo kifundo cha mguu, funiko la mguu, kisigino, vidole vya miguuni na ligamenti ya kisigino.

Eneo la mguuni huwa na kazi kubwa ya kunyonya shinikizo kubwa la uzito wote wa mwili na hii ndiyo sababu eneo hilo kupata majeraha kirahisi.

Hali hii huchangia kujijeruhi mara kwa mara hata kabla ya jeraha kupona vizuri jambo ambalo linachangia eneo kuwa na maumivu sugu au kuchelewa kupona.

Ni vigumu kwa mwanamichezo kuepuka majeraha ya sehemu ya chini mguu katika kifundo kuelekea katika funiko la mguu kwani ndilo eneo ambalo lina harakati nyingi wakati wa kucheza au mazoezi.

Kifundo cha mguu ndiyo sehemu ya mguuni ambayo inapata sana majeraha na kusababisha kuwapo kwa maumivu sugu kwa wanamichezo kutokana na kuchelewa kupona.

Wakati wa mazoezi au kucheza ni kawaida mguu kutua vibaya na kujipinda eneo la kifundo hivyo kujeruhi tishu laini ikiwamo nyuzi za ligamenti ambazo hujivuta kupita kiasi.

Tishu laini za mguuni zinaweza kujeruhiwa kwa kuminywa, kujipinda, kunepa, kuvutika kuliko pitiliza , kukwanyuka, kuchubuka, kuchanika kiasi au kukatika na kuachana pande mbili.

Hali hii inaweza kusababisha eneo la ungio la mguu hasa katika kifundo kupata maumivu, kuvimba na kushindwa kufanya matendo mbalimbali ikiwamo kutembea.

Vile vile maumivu sugu ya mguu yanaweza kusababishwa na majeraha katika mifupa midogo ya miguu ikiwamo nyufa, kututumka, na kuvunjika vifupa vidogo ikiwamo vya vidoleni.

Hatua kadhaa zinaweza kufanyika ili kukabiliana na maumivu sugu ya eneo hili ikiwamo kuhakikisha kuwa unapumzika na kuacha kujishughulisha na chochote mpaka pale itakapothibitika umepona.

Wanamichezo waepuke kuanza mazoezi kabla ya kupona vizuri kwani kunachangia kuongeza ukubwa wa jeraha au kulitonesa jeraha.

Matumizi ya dawa za maumivu kiholela yaepukwe kwani kuzitumia kwa muda mrefu ni chanzo cha kutopona jeraha na kuendelea kupata maumivu.

Wakati mwingine matibabu salama ya nyumbani ni mbadala mzuri wa dawa za maumivu, tumia matibabu salama maumivu ya mguu kwa kupumzika, kuweka barafu, kuugandamiza na bandeji ya kupana na kuunyanyua kuzidi kifua.

Kama unapata maumivu sugu ni muhimu kutathimini aina ya mazoezi unayofanya au kupewa kwani mazoezi magumu yanasiyo na kipimo yanaweza kuchangia tatizo hili.

Fanya chaguzi sahihi ya viatu unavyotumia kufanyia mazoezi au kuchezea kwani baadhi ya viatu si sahihi kwa michezo na hakikisha unakimbilia maeneo ambayo ni tambarale.



Chanzo: mwananchi.co.tz