Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matumizi ya simu, daktari aonya

Fri, 14 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unguja.Mratibu wa afya ya akili Zanzibar, Dk Sleiman Abdu Ali ameitahadharisha jamii kujiepusha na matumizi ya simu kupitiliza kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha ugonjwa wa akili.

Amesema miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la watumiaji wa simu za mkononi hususani vijana kiasi kwamba baadhi yao hushindwa kupumzika hasa wakati wa usiku wakati wote wakiwa wanatumia simu.

Akizungumza na Mwananchi mjini hapa jana, daktari huyo alisema baadhi ya watu muda wao mwingi wamekuwa wakitumia simu kuliko kufanya shughuli nyingine ikiwamo kulala hali ambayo inahatarisha afya yao ya akili.

“Ongezeko la matumizi ya simu baadhi ya wakati huwafanya vijana wetu kuona kama hawana usingizi kutokana na mawazo yote kuwa ndani ya simu kwa kuchati au kuongea mchana na usiku,” alisema.

Alisema licha ya teknolojia ya simu kuwa nzuri katika kupeana habari pamoja na kufikishiana ujumbe, lakini baadhi ya watu wamekuwa wakitumia kupita kiasi.

“Wale ambao wanaendekeza matumizi ya simu kupita kiasi wajiandae na maradhi mbalimbali ikiwamo ugonjwa akili,” alisema.

Dk Ali alisema jamii inapaswa kujiepusha na matatizo hayo na kujipa muda wa kutosha wa kupumzikaili kujiepusha na magonjwa hayo.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi visiwani hapa walisema ni kweli vijana wengi hupenda kutumia simu za mkononi muda mwingi kuliko kulala.

Mwanaidi Khamis alisema yeye binafsi baadhi ya siku hufika hadi saa nane usiku bila ya kupata usingizi huku shughuli kubwa anayofanya ni kuchati na kuangalia mitandao ya kijamii.

Naye Haji Mwadini alisema matatizo ya kimaisha ambayo yamekua yakiwakumba baadhi ya wananchi sababu kubwa ni kukosa usingizi na kutumia muda mwingi kuwaza.

Kwa sharti la kutotajwa jina, mtaalamu wa afya Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mjini hapa alisema mara kadhaa wamepokea wagonjwa wakiwa na matatizo ya kukosa usingizi kunakosabishwa na matumizi ya simu kwa muda mrefu hasa nyakati za usiku.



Chanzo: mwananchi.co.tz