Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matumizi ya kiboko sio jibu kwa mtoto aliyekosa nidhamu

15593 Cristian+Bwaya TanzaniaWeb

Tue, 4 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tumezoea kuadhibu watoto wetu kwa kuwachapa. Tunapowaambia kitu na hawaonekani kusikia, wazazi wengi tunafanya haraka kutumia kiboko kama mkakati wa ‘kumnyoosha’ mtoto. Lakini je, kiboko kinasaidia?

Katika utafiti mmoja, wazazi walitengwa katika makundi mawili kutegemeana na kiwango chao cha hasira. Wazazi hawa walipowekewa mazingira ya kuwaadhibu watoto wao kwa makosa yanayofanana, tofauti ilikuwa bayana.

Wazazi wenye hasira walikuwa wepesi kufoka na kutumia mabavu wakati wenzao wenye kiwango cha chini cha hasira walitumia mbinu rafiki kuwarekebisha watoto wao.

Mara nyingi mzazi anapomchapa mwanawe hufikiri anafanya hivyo kwa nia ya kumsaidia mtoto. Lakini utafiti huu unatusaidia kuelewa kuwa mzazi asiye na hasira hawi na msukumo wa kutumia fimbo kuliko mwenzake mwenye hasira. Maana yake ni kwamba lazima iwepo sababu nyingine zaidi ya ‘kumnyoosha mtoto.’ Kisasi kinaweza kuwa sababu mojawapo.

Mzazi mwenye hasira anapobaini mwanawe anatenda kinyume na matarajio yake, hughadhibika. Nafsi yake hujisikia kudhalilika.

Katika mazingira haya, mzazi wa namna hii anapomchapa mtoto kimsingi anajisaidia mwenyewe kupunguza hasira zake. Hiki ni kisasi ambacho kikichunguzwa vyema, hakina lengo la kurekebisha tabia ya mtoto bali kupunguza hasira.

Wengi tuliosoma kwenye shule za kawaida ni mashuhuda wa hali hii. Walimu waliokuwa na hasira wengi wao ndio hasa waliopenda kuchapa. Hawakutuchapa kwa nia ya kutusaidia.

Wakati mwingine, walifanya hivyo kutuonyesha kuwa hatuwezi kuwachezea. Walimu hawa walitumia viboko kama namna ya kupooza hasira zao na sio kuturekebisha.

Mara nyingi nimeongea na wazazi na walimu kuhusu adhabu ya kiboko. Ninapowasikiliza ninabaini kwamba wazazi wengi wamefika mahali wanaamini fimbo kuliko hata nidhamu yenyewe ya mtoto. Fimbo inachukuliwa kuwa alama ya malezi hata kama faida zake haziko wazi.

Inawezekana kuna suala la mazoea. Wapo wazazi wanaopenda kusema, “Nimefika hapa kwa sababu ya fimbo! Bila fimbo nisingefika hapa nilipo.” Huwa nikisikia utetezi wa namna hii, najiuliza mantiki yake hasa ni ipi? Kwa nini mtu aamini fimbo ndizo zilizochangia mafanikio yake? Hivi unajuaje kuwa usingechapwa usingefanikiwa?

Kama ambavyo wapo wengi wasiochapwa na wakaharibika, wapo pia waliochapwa na wakaharibika.

Huwezi kuhitimisha tu kuwa kwa kuwa wapo waliofanikiwa na walichapwa basi kilichowafanikisha ni fimbo. Lazima iwepo sababu zaidi ya fimbo.

Kimsingi, nafasi ya fimbo kwenye malezi katika mazingira haya inakuwa ni imani tu. Ni mwendelezo wa utamaduni tulioukuta na tunafikiri unatufaa. Na kwa sababu hatufahamu mbadala wake, basi tunajisikia kuwajibika kuuendeleza vile ulivyo.

Wengine wanatumia vitabu vya dini kuhalalisha fimbo. Lakini kuna ukweli pia kuwa mara nyingi tunachapa kwa mazoea tu ya mila tunayoamini ni sahihi.

Dini ni namna tu ya kuhalalisha mazoea yetu ambayo tungeyaendeleza hata kama hayajazungumzwa kwenye vitabu vya dini. Kwa kuwa hatuwezi kukubali kuwa kuchapa ni kujiridhisha wenyewe, basi tunatumia mafundisho ya dini kama mwamvuli.

Pamoja na utetezi wa fimbo, yapo madhara mengi. Moja, tumesikia visa vya wanafunzi kupoteza maisha shauri ya vipigo vya walimu wao. Ingawa ni rahisi kusema kilichofanyika ni zaidi ya kuchapa, bado ni ukweli kuwa mstari kati ya adhabu ya fimbo na ukatili ni mwembamba.

Ni vigumu, kwa mfano, kujua faida ya adhabu ya viboko inaishia wapi na ni kuanzia wapi adhabu hiyo hugeuka kuwa ukatili.

Fikiria jambo hili. Fimbo zina tatizo la kuzoeleka. Kadri inavyotumika kumsababishia maumivu mtoto, ndivyo inavyobidi iwe kali zaidi.

Isipokuwa kali na nzito haiwezi tena kuendelea kumfanya mtoto apate maumivu yanayotarajiwa. Kama mtoto alikuwa akichapwa fimbo mbili ndogo, baada ya muda, fimbo mbili hazitoshi kumpa wasiwasi. Anajua akikosea, atapata fimbo mbili na mambo yataisha.

Kwa kuwa mzazi hana namna nyingine ya kumrudi mwanawe, mtoto hufanya kosa lilelile.

Mzazi naye hutumia mbinu ileile ya kumsababishia mtoto maumivu akifikiri anaweza kumjengea hofu ya kutorudia alichokifanya.

Kwa mshangao wake, anakuta mtoto hatetemeki tena aonapo fimbo.

Suluhu inakuwa ni kuongeza mapigo ili kutengeneza woga unaoonekana kupotea.

Kadri mapigo yanavyozidi kuongezeka na kuwa makali zaidi, ndivyo adhabu inavyoendelea kupoteza maana yake na kugeuka kuwa ugomvi kati ya mzazi na mtoto.

Mazingira kama haya ndiyo yanayofanya wakati mwingine walimu na wazazi kujikuta wakiwafanyia ukatili watoto wao bila wao wenyewe kujua wanachokifanya.

Ukiacha hilo la fimbo kugeuka kuwa udhalilishaji, anayechapwa naye anajifunza kuwa mbabe. Watoto wanaochapwa, mara nyingi huwa ni wagomvi katika maisha halisi.

Hujikuta wakiwa na mazoea ya kupigana na wenzao na hata watu wengine kama namna ya kutatua matatizo yao.

Tabia ya ugomvi anakuwa amejifunza kwa wazazi wake mwenyewe. Amemwona baba akishika fimbo kushughulikia tatizo na yeye atamshika shati mtu mwingine anayemkosea. Hawezi kuona njia nyingine bora zaidi. Mtoto wa nyoka anaendelea kuwa nyoka.

Matokeo ya mazoea haya ni kumfanya awe mtu wa mabavu, mchokozi kwa wenzake, asiyeweza kuelewa hisia za wengine na mwisho wake na yeye wenyewe hugeuka kuwa mtu anayeunga mkono fimbo kwa watoto wake. Ni mwendelezo wa utamaduni wa ubabe.

Ninachojaribu kukisema ni hiki: kiboko hakiwezi kuwa jibu la nidhamu ya mtoto. Maumivu anayoyapata mtoto kwa kiboko hayawezi kumfanya akawa na msukumo wa dhati ya kumsikiliza mzazi. Tufanyeje basi?

Napendekeza njia mbadala. Badala ya kumuumiza mtoto kwa kumtisha na kumchapa, jaribu kufanya jitihada za kujua kwa nini hasikii kile unachotaka akisikie. Je, inawezekana makosa yako ndiyo yanayosababisha makosa unayoyaona kwa mwanao? Unakosea wapi?

Je, inawezekana ulipuuza dalili na sasa unajaribu kutumia njia ya mkato kutatua tatizo kubwa?

Je, inawezekana unalazimika kutumia mabavu kwa sababu hujawekeza kwenye ukaribu unaomfanya mwanao asukumwe kukuheshimu?

Chanzo: mwananchi.co.tz