Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matumizi ya heroin, cocaine yapungua Tanzania

Fri, 11 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkemia Mkuu wa Serikali nchini Tanzania, Dk Fidelice Mafumiko amesema matumizi ya mihadarati aina ya heroin na cocaine yamepungua kwa kiasi kikubwa kutoka mwaka 2015 hadi 2018 huku matumizi ya bangi na mirungi yakiongezeka.

Akizungumza leo Alhamisi Januari 10, 2019 wakati wa ziara ya maofisa wa habari wa Wizara ya Afya kwa taasisi zake, Dk Mafumiko amesema Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imefanikiwa kupitia ushirikiano baina yao na taasisi zingine.

Amesema uwekezaji wa mitambo ya kisasa kubaini sampuli kwa muda mfupi umesaidia kurahisisha utendaji kazi wa taasisi hiyo.

“Udhibiti umekuwa mkubwa hapa nchini lakini pia mamlaka tumepigana vita kupambana na dawa za kulevya na kupambana na uhalifu nchini, udhibiti wa dawa za kulevya umedhihirika kwa kadri sampuli zinazoletwa kuongezeka na hiyo inaonyesha kudhibiti,” amesema.

“Mwaka 2018 sampuli ziliongezeka hadi kufikia 88,890 sawa na asilimia 90 na zote zilifanyiwa uchunguzi na kuonyesha matokeo yake na kusaidia kuondoa tatizo hilo.”

Dk Mafumiko amesema sampuli 96,284 kutoka Jeshi la Polisi zilitolewa majibu.

Amesema ikilinganishwa na miaka iliyopita, matumizi ya mihadarati yanapungua kwa kasi kubwa hivyo kuonyesha namna ambavyo mamlaka husika zimepambana kuondoa tatizo hilo.

“Ukilinganisha mwaka 2014 zaidi ya asilimia 50 ya sampuli za dawa za kulevya zilizoletwa (katika) mitambo yetu ilibaini zilikuwa ni heroin, lakini mwaka 2015 ilipungua kidogo,” amesema.

Amesema mwaka 2016 bangi ilianza kuchukua nafasi kubwa na kufikia asilimia 68 na mwaka 2017 ikafikia asilimia 80 huku heroin ikishuka hadi asilimia 12 na cocaine ikiwa chini ya asilimia moja.

Amesema kila siku mamlaka hiyo inapokea sampuli kutoka polisi na nyingi ni za mihadarati na dawa za kulevya pamoja kesi za vinasaba.

Dk Mafumiko amesema mafanikio hayo yametokana na kuimarishwa pia kwa mamlaka hiyo kwa kuwa na mitambo ya kisasa inayotoa majibu kwa muda mfupi.

“Tunao mtambo mkubwa na wa kisasa unaozidi Sh1.6 bilioni unaotuwezesha kuchunguza sampuli na vielelezo mbalimbali vya dawa za kulevya, chakula na vinginevyo wenye uwezo mkubwa ikilinganishwa na mitambo mingine tuliyonayo nchini.”

Amesema mtambo huo una uwezo wa kuchunguza sampuli nyingi kwa muda mfupi.

“Mtambo huu sampuli ya damu inachunguza kwa muda wa saa moja huku mitambo mingine tuliyonayo inachukua wiki mbili hadi tatu, dawa za kulevya unatoa matokeo ndani ya dakika 40 wakati mitambo mingine inachukua wiki 3,” amesema.

Naye kaimu mkurugenzi wa idara ya usimamizi wa kemikali, Daniel Ndiyo amesema mamlaka hiyo inapokea sampuli mbalimbali kwa ajili ya uchunguzi zikiwemo za watu binafsi huku nyingi zaidi zikiwa ni za serikali.

“Sampuli za dawa za kulevya lazima zidhibitishwe hapa lakini pia za jinai, mamlaka yetu pia inafanya uchunguzi wa jinsia kwa kushirikiana na madaktari,” amesema.

Amesema mamlaka hiyo kwa sasa imeanza kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili kupata ufumbuzi wa kugundua jinsia na pia uchunguzi wa matibabu ya figo unategemea vipimo vya uhusiano wa mtoaji na anayepokea.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz