Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matumaini mapya kwa wenye VVU

9569 Ukimwi+pic TZWeb

Wed, 20 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma.  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Watoto na Wazee, Ummy Mwalimu amesema Serikali itaanza kutoa dawa mpya za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARVs) itakayokuwa na ufanisi zaidi kuliko inayotumika hivi sasa nchini.

Ummy ameyasema hayo leo Juni 19 2018 katika uzinduzi wa kampeni ya Furaha Yangu, Pima, Jitambue, Ishi, inayolenga kuhamasisha watu hasa wanaume kupima VVU kwa hiari na kuanza matumizi ya dawa za kufubaza makali ya ugonjwa Ukimwi (ARVs)

“Tutaanza kutoa dawa mpya za ARVs kwa watu wanaoishi na VVU ambazo zina ufanisi mkubwa na zinapunguza maudhi kwa watumiaji,”amesema.

Ummy pia amesema wameanza majaribio ya kutoa dawa za ARVs kwa miezi mitatu kwa watu ambao mwenendo wao wa matumizi ya dawa hizo unaridhisha badala ya mwezi mmoja.

Amesema mpango huo wa kutoa dawa kwa miezi mitatu hautawahusu wajawazito, watoto na wale ambao mwenendo wao wa utumiaji ARVs hauridhishi.

Ummy amesema pia wamepanga kuongeza vituo vya kutoa huduma kwa watu wanaoishi na VVU ambapo hadi kufikia Desemba mwaka huu vitafikia 4,050 kutoka 1,866 vilivyopo sasa.

Kuhusu upatikanaji dawa za kutibu magonjwa nyemelezi, Ummy amesema kuwa katika bajeti ya mwaka 2018/19 wametenga Sh 5.3 bilioni kwa ajili ya kununua dawa za kutibu magonjwa nyemelezi nchini kati ya Sh 266bilioni zilizotengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz