Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matibabu saratani shingo ya kizazi kutolewa bure

Mon, 18 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Baraza la Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Kilimanjaro kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Taasisi la Saratani ya Ocean Road pamoja na Kikundi cha Ugweno watatoa matibabu bure kwa wagonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi na matiti kwa wanawake.

Katibu wa Bakwata Kilimanjaro Awadh Lema alisema jana kuwa matibabu hayo yatatolewa Juni 30 mwaka huu na wanakusudia kutoa huduma hiyo kwa wanawake zaidi ya 200.

Pia, alisema watashirikiana na madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi.

Alisema saratani ya shingo ya kizazi na matiti inaweza kutibika kwa gharama nafuu endapo watawahi mapema kupima afya zao kabla ya tatizo hilo kuwa kubwa.

Lema aliwataka wanawake kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili kupima afya zao na kusaidia kupunguza ongezeko la ugonjwa huo.

“Sote tunatambua kuwa saratani ya shingo ya kizazi na matiti ni tatizo kubwa kwa wanawake na tayari ugonjwa huu umesababisha vifo vingi,” alisema Lema.

Alifafanua kuwa Bakwata wanaunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na ugonjwa huo.

Baadhi ya wanawake walisema huduma hiyo itawasaidia kujua afya zao na kuchukua tahadhari mapema kabla tatizo halijawa kubwa.

“Saratani ya matiti na shingo ya kizazi imewatesa wanawake wengi na wengine hufika hospitali wakati tatizo ni kubwa, nipongeze Bakwata kwa kuliona hili kwani huduma watakayoitoa itasaidia wanawake wengi,” alisema Rose Mongi.

Inaelezwa kuwa saratani ya shingo ya kizazi inashika nafasi ya pili miongoni mwa saratani zinazogharimu maisha ya wanawake duniani kote.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa takribani vifo 500,000 vya wanawake hutokea kila mwaka kutokana na saratani hiyo hasa katika nchi za Afrika ikiwamo Tanzania.

Miezi kadhaa iliyopita Serikali imeanza kutoa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi ya Human Pappilloma Virus (HPV) kwa wasichana wenye miaka kati ya tisa na 14 ili kuwakinga na ugonjwa huo.

Chanzo: mwananchi.co.tz